WAKATI timu zao zikikaribia kuanza maandalizi ya msimu mpya, Dodoma Jiji na Pamba Jiji zimefanya uamuzi unaofanana kama majina yao yalivyo mwishoni.
Zote zimevunja mabenchi yao ya ufundi ambayo yameziongoza timu hizo katika msimu uliopita na zimeingiza sura mpya ambazo zitazinoa katika msimu unaokuja wa 2025/2026.
Dodoma Jiji imeachana na Mecky Maxime aliyeiongoza timu hiyo kumaliza katika nafasi ya 12 katika msimamo wa Ligi Kuu msimu jana huku Minziro akiiwezesha Pamba Jiji kumaliza katika nafasi ya 11.
Sisi hapa kijiweni hatujui nini ambacho kimesababisha timu hizo mbili kuachana na makocha hao ambao wameziwezesha kutimiza lengo lao la msingi ambalo ni kubakia katika Ligi Kuu. Huo ndiyo ukweli, tusiaminishane zilikuwa na lengo la kutwaa ubingwa.
Lakini hadi uongozi umeamua kutoendelea nao, kuna sababu zao ambazo zimechangia hilo na inawezekana pia pengine ni makocha wenyewe wameomba kuachana na timu hizo ili wakasake malisho ya kijani zaidi mahali kwingine.
Hata hivyo, vyovyote itakavyokuwa, kijiwe kinaamini mafundi hawalali na njaa na hivyo ndivyo kinavyotegemea kwa Maxime na Minziro hawawezi kukaa msimu mzima bila kuwa na timu ya kufundisha.
Inawezekana wakapata timu kipindi hikihiki cha kabla ya msimu kuanza kwani ni makocha wenye uzoefu mkubwa na soka la bongo na wana sifa stahiki za kuwa makocha wakuu tofauti na ilivyo kwa wazawa wengi.
Lakini kama ikishindikana kwa sasa basi wakati msimu utakapokuwa ukiendelea, kuna uwezekano mkubwa Maxime na Minziro wakaibukia hapo hasa kwa timu ambazo zitakuwa katika uwezekano wa kushuka daraja.
Hawa ni makocha ambao kwa nyakati tofauti wameonyesha uwezo wa kuziokoa timu ambazo zilikuwa katika hali mbaya kwenye ligi na zinanyemelea kushuka daraja kwa kuzitoa hapo na kuziwezesha kubakia kwenye ligi.
Mfano ni huyohuyo Minziro kwa Pamba Jiji na aliikuta ikiwa haijapata ushindi hata chembe kwenye ligi na ipo katika nafasi mbaya na kuisogeza juu hadi ikanusurika na janga la kushuka ambalo likazikumba Kengold na Kagera Sugar.