KAMISHENI ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBRC) imesema ili kuhakikisha mchezo huo unafika mbali wanapaswa kutambua na kufahamu rekodi za afya za mabondia kabla na baada ya kupigana.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Kamisheni hiyo, Emmanuel Saleh wakati alipokuwa katika hafla ya kusaini mkataba wa miaka mitatu na hospitali ya Hitech Sai wenye lengo la kutoa huduma za afya kwa mabondia waliopo chini ya TPBRC.
Amesema hiyo ni fursa kwao kwani, kilikuwa kilio cha muda mrefu kutafuta kituo cha afya kitakachokuwa kinawasaidia ili kujua afya za mabondia pamoja na matatizo mengine.
“Tumeingia sehemu salama, ikiwa ni mara ya kwanza kupata kituo kikubwa cha afya kama hiki ambacho kitakuwa kinatusaidia kupima afya za mabondia kabla na baada ya pambano,” amesema Saleh.
Amesema wapo tayari kushirikiana nao kwani, wanafahamu thamani ya bondia kupima afya kwa kuwa utawasaidia kwa kiasi kikubwa.
Kwa upande wa Mtendaji Mkuu wa Hospitali ya Hitechi Sai, Gean Cabral amesema ameamua kuingia mkataba huo kutokana na kutambua thamani ya mchezo wa ngumi hapa nchini.
“Lengo la mkataba huu ni kuhakikisha afya za mabondia zinakuwa salama muda na wakati wowote kwa lengo la kuupeleka mbali zaidi,” amesema Cabral.
Aidha amesema mbali na mchezo wa ngumi vile vile wanawasaidia wachezaji wa mchezo wa kuogelea pamoja na ule wa Kriketi.