TRA YATOA MSAMAHA WA KODI KWA WAMILIKI WA MAGARI YASIYOKIDHI MATAKWA YA FORODHA

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imetoa msamaha wa kodi kwa wamiliki wa magari yasiyokidhi matakwa ya forodha kwa kipindi cha kuanzia Agosti mosi hadi Disemba 31 mwaka huu.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na TRA leo Agosti Mosi Jijini Dar es Salaam na kusainiwa na Kamishna Mkuu Bw. Yusuph Juma Mwenda imeeleza kuwa katika kipindi cha msamaha, wamiliki wa magari husika watawajibika kulipa kiasi cha ushuru na kodi husika, bali kiasi cha riba na adhabu vyote vitasamehewa.

Taarifa hiyo imesema ‘TRA katika kutekeleza majukumu yake yaliyokasimiwa kwa mujibu wa Sheria ya Mamlaka ya Mapato Tanzania, Sura 399 (kama ilivyofanyiwa marejeo), imekuwa ikikabiliana na changamoto za usimamizi wa magari yasiyokidhi matakwa ya Sheria ya Forodha (uncustomed vehicles), ambayo hayakulipiwa ushuru na kodi husika wakati wa kuingizwa nchini. 

Pia, Magari yaliyoingizwa nchini kwa muda (temporary importation) na hayakuweza kurudishwa yalikotoka.

Vilevile,Magari yaliyoingia Tanzania Bara kutokea Zanzibar bila kufuata taratibu za kiforodha, magari yaliyoingizwa nchini kwenda nchi nyingine (transit) na yakabakizwa au kutelekezwa nchini.

Pia, Magari yaliyosamehewa kodi lakini umiliki wake umehamishiwa kwa watu wasiostahili kupewa msamaha.

Pia, changamoto nyingine ni katika magari yaliyoingizwa nchini kwenda nchi nyingine ambayo muda wake umeisha na hayakupata kibali cha nyongeza.

Taarifa imeeleza kwa mujibu wa Kifungu cha 70(1) cha Sheria ya Usimamizi wa Kodi Sura 438 na Kifungu cha 249 cha Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya mwaka 2004, Kamishna Mkuu wa Mamlaka anatoa Msamaha wa kodi (AMNESTY) kwa wamiliki wa magari ambayo yaliingizwa nchini kwa kujua au kutokujuwa kwamba hayakulipiwa ushuru na kodi husika kikamilifu.

Taarifa imeeleza kuwa msamaha huo wa kodi utakuwa kwa kipindi cha kuanzia Agosti mosi 2025 hadi Disemba 31 2025 na utahusu magari yaliyoingizwa nchini Tanzania bila kukidhi matakwa ya Sheria. 

Imesema katika kipindi cha msamaha, wamiliki wa magari husika watawajibika kulipa kiasi cha ushuru na kodi husika, bali kiasi cha riba na adhabu vyote vitasamehewa.

“Hivyo wamiliki wanatakiwa kufika katika ofisi za TRA zilizo karibu nao wakiwa na ushahidi wa umilki pamoja na nyaraka za uingizwaji nchini wa magari husika, kwa ajili ya kukadiriwa ushuru na kodi stahiki,” imeelezwa. 

Taarifa imeeleza kuwa magari yaliyo kwenye makundi tajwa yatakayokamatwa baada ya tarehe 31 Disemba, 2025 ambayo ushuru na kodi zake hazikulipwa kikamilifu yatashughulikiwa kwa mujibu wa Sheria.

“Mbali na mashtaka ya jinai, watawajibika kulipa ushuru na kodi ikiwa ni pamoja na riba na adhabu,” imeeleza taarifa ya Kamishna Mwenda.

Mwisho