Dar es Salaam. Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (Tira) imesaini Hati ya Makubaliano (MoU) na Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) yenye lengo la kuweka mazingira wezeshi kwa ajili ya kukuza bidhaa za kifedha bunifu, hasa suluhisho za bima zinazoweza kuorodheshwa sokoni, sambamba na kuboresha elimu ya fedha kwa umma.
Akizungumza Ijumaa, Julai 31, wakati wa hafla ya utiaji saini, Kamishna wa Bima Dk Baghayo Saqware alielezea ushirikiano huo kama hatua ya kimkakati ya kupanua fursa kwa makampuni ya bima kupata mitaji kupitia soko la hisa, huku wakilinda maslahi ya walaji na kuongeza ufanisi wa kifedha.
Dk. Saqware alisisitiza kuwa kupitia ushirikiano huu, taasisi zote mbili zinalenga kuimarisha mzunguko wa taarifa kati ya Tira na DSE kwa ajili ya kurahisisha usimamizi na uchambuzi wa takwimu, kusaidia kampuni za bima kuchangia katika soko la mitaji kwa kuorodhesha dhamana zao, na kufanya tafiti pamoja pamoja na mafunzo ya kitaalamu.
Aliongeza kuwa Tira inaamini mafanikio ya sekta ya bima hayawezi kutenganishwa na nguvu ya masoko ya mitaji, na kwamba sekta hizi mbili kwa pamoja zinaweza kujenga mfumo imara na jumuishi wa kifedha wenye manufaa kwa Watanzania wote.
Makubaliano haya yamekuja katika kipindi ambacho sekta ya bima Tanzania imeonyesha ukuaji mkubwa. Kwa mujibu wa takwimu za karibuni za Tira, idadi ya watu waliokatiwa bima iliongezeka kutoka milioni 17 mwaka 2022 hadi zaidi ya milioni 25 mwaka 2023, huku bima ya afya ikifunika asilimia 37 ya wananchi.
Idadi ya watoa huduma wa bima pia iliongezeka zaidi ya mara mbili kutoka 993 mwaka 2021 hadi 2,208 mwaka 2024, na ajira katika sekta hiyo zilifikia watu 6,916. Huku upenyezaji wa bima (insurance penetration) ulipanda kutoka asilimia 0.56 mwaka 2021 hadi asilimia 2.01 mwaka 2023 ya Pato la Taifa (GDP).
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa DSE, Peter Nalitolela, alisema makubaliano hayo ni sehemu ya mkakati mpana wa kuunganisha sekta za bima na soko la mitaji nchini Tanzania.
Alifafanua kuwa MoU hiyo ni ramani ya jinsi ambavyo sekta hizi mbili zitashirikiana ili kuboresha ujumuishaji wa kifedha, kuongeza uwazi, na kuchochea mageuzi ya kiuchumi kulingana na Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050.
Nalitolela aliongeza kuwa ushirikiano huo utasaidia katika kukuza rasilimali watu, kuendeleza ubadilishanaji wa maarifa kati ya taasisi hizo, na kuimarisha sekta ya umma na binafsi.
“Mkataba huu wa makubaliano ni ishara ya kimkakati kwa sekta hizi mbili kubwa za kifedha hapa nchini. Itasaidia kutoa namna ya kuongeza ujumuishi wa kifedha hapa nchini, kuboresha uwazi na kuchochea kasi ya maendeleo ya uchumi,” anasema
Alifafanua kuwa ushirikiano huo utahusisha kuandaa matukio ya kitaalamu ya pamoja yanayowakutanisha wadau muhimu kutoka sekta za bima, masoko ya mitaji, na jamii ya wawekezaji, kwa lengo la kuendeleza ubunifu, kuboresha mbinu za usimamizi wa hatari, na kusaidia ukuaji wa mazingira thabiti na yanayotarikika ya kiuchumi.