Kibaha. Siku chache kabla ya kura ya maoni ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM), wagombea watatu wa ubunge Jimbo la Kibaha Vijijini, mkoani Pwani, leo Ijumaa Agosti Mosi, 2025, wameendelea kujinadi kwa wajumbe wa mkutano mkuu wa chama ngazi ya kata.
Wakiwa katika Kata ya Kilangalanga, wagombea hao ambao ni mbunge aliyemaliza muda wake, Michael Mwakamo, Hamood Jumaa na Eli Achahofu wamepewa dakika tatu kila mmoja kuwasilisha sera zao na dakika tatu za kujibu maswali kutoka kwa wajumbe.
Akizungumza katika muda huo aliopewa, Mwakamo amewaomba wajumbe wamrejeshe kwa kipindi cha pili ili amalizie kazi aliyoianza.
“Mlinituma kwa miaka mitano, nimefanya mengi kwa kufuata Ilani ya chama. Naomba mnirudishe tena niendelee kuwatumikia,” amesema Mwakamo.

Wajumbe wa CCM Kata ya Kilangalanga Wilaya ya Kibaha Vijijini Mkoa wa Pwani wakisikiliza sera za mmoja wa wagombea. Picha na Sanjito Msafiri
Kwa upande wake, Hamood Jumaa amejieleza kama kiongozi anayezielewa changamoto za wananchi na mwenye dhamira ya kuzitatua.
“Nina ndoto ya kuona Kibaha Vijijini inasonga mbele. Nawaomba mniamini, mnitume nikawatumikie kwa moyo mmoja,” amesema kwa kujiamini.
Naye Eli Achahofu, amesema dhamira yake ni kupunguza kero kwenye sekta ya miundombinu, elimu na uchumi.
“Barabara zetu ni changamoto, huduma za elimu na fursa za kiuchumi bado ni finyu. Nikiwa mbunge, nitahakikisha haya yanatatuliwa,” amesema Achahofu.
Mapema, Katibu wa CCM Wilaya ya Kibaha Vijijini, Ezekiel Mollel amewataka wajumbe kufuata kanuni na taratibu za uchaguzi ndani ya chama, akisisitiza umuhimu wa umoja.
“Mmeona wenyewe, wagombea wote wamefika hapa kwa gari moja, wanakula chakula kimoja, hii ni dalili ya mshikamano. Hivyo, nasi kama wajumbe hatuna sababu ya kugawanyika,” amesema Mollel.
Kura ya maoni ya kumpata mgombea mmoja atakayepeperusha bendera ya CCM inatarajiwa kupigwa Agosti 4, 2025.