Wanaotarajia kusoma elimu ya juu wakumbushwa kuzingatia soko la ajira

Pemba. Wanafunzi wanaofanya usaili kujiendeleza na elimu ya juu, wametakiwa kuwa makini katika kuhakikisha wanachukua fani zinazoendana na soko la ajira.

Ushauri huo umetolewa na mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia kutoka mkoani Mbeya, Dk Faston Mayala katika maonyesho ya wiki ya elimu ya juu yaliyofanyika Gombani Kisiwani Pemba.

Amesema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ya Zanzibar, mara nyingi zimekuwa zikitilia mkazo masomo ya sayansi kutokana na uhitaji wa fani za masomo hayo, hivyo wanafunzi hawana budi katika kuangalia fani zinazoendana na wakati.

Amesema masomo ya sayansi yanakuwa na nafasi kubwa katika soko ya ajira na kama mwanafunzi, atajikita katika fani za masomo hayo anaweza kuingia katika soko la ajira.

“Niwashauri wanafunzi wanaofanya udahili wa kujiendeleza katika elimu ya juu, wanapaswa kuwa makini katika kuchagua fani inayoenda na soko la ajira,” amesema Dk Mayala.

Ofisa Mdhamini kutoka Wizara ya Elimu na Mafuzo ya Amali Pemba, Mohamed Nassor Salum, amesema maonyesho hayo yanalenga kuwasogezea karibu huduma za kielimu kwa wanafunzi.

Amesema maonyesho ya elimu ya juu yamekuwa yakifanyika kila mwaka katika Visiwa vya Unguja na Pemba ili kuwarahisishia wanafunzi kufanya maombi na kujiunga na elimu ya juu.

“Wizara ya Elimu imekuwa ikifanya maonyesho hayo kwa lengo la kuwafikishia huduma za elimu kwa wanafunzi hasa wanaotaka kujiunga na elimu ya juu,” amesema.

Amesema wizara imekuwa ikifanya hivyo ili huduma ziwafuate wanafunzi badala ya wao kuzifuata.

“Serikali imekuwa ikifanya maonyesho hayo kwa lengo la kuwasogezea karibu huduma za elimu kwa wanafunzi wanaotaka kujiendeleza elimu ya juu,” amesema.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (Suza), Hamid Mselem Salum ameipongeza Serikali katika kuweka maonyesho hayo ambayo yanatoa fursa mbalimbali kwa wanafunzi.

Amesema yamewasaidia wanafunzi changamoto hasa katika uombaji wa mikopo na vyuo wanavyotaka kujiendeleza.

Kauthari Mohamed ni mwanafunzi aliyefika katika maonyesho hayo amesema kuwepo kwa maonyesho hayo kunawapa fursa katika kuchagua sehemu sahihi ya kujiendeleza kielimu.

“Haya maonyesho ni muhimu sana, yanasaidia kujua vitu vingi, kupewa maelekezo na miongozo, hakika tunashukuru sana,” amesema.