Yanga kazi imeanza! | Mwanaspoti

MABOSI wa Yanga wameshamaliza kazi ya kusajili majembe ya maana kwa kikosi cha msimu ujao wa mashindano, ikiwamo kushusha makocha wapya katika benchi la ufundi na leo benchi hilo chini ya kocha Romain Folz linaanza rasmi kazi ya kukinoa kikosi hicho kwa maandalizi ya msimu mpya.

Ndio, kazi inaanza rasmi leo na presha katika klabu hiyo sasa inahama kwa Folz na jopo lake baada ya viongozi kukamilisha kazi ya usajili na kivitendo vinaanza kwenye Uwanja wa KMC Complex, jijini Dar es Salaam.

Ipo hivi. Kocha Folz na jopo lake leo linaanza rasmi kazi baada ya wachezaji wapya na wale wa zamani kufanyiwa vipimo kwa siku mbili juzi na jana, ili kuanza kujifua tayari kwa ajili ya kujiandaa na msimu mpya sambamba na mechi ya kirafiki na Rayon Sport Agosti 15.

Chanzo cha kuaminika kutoka Yanga kimeliambia Mwanaspoti kikosi cha Yanga chote leo Ijumaa kitatakiwa Uwanja wa KMC Complex tayari kwa ajili ya maandalizi.

“Juzi na jana tumekamilisha zoezi la vipimo kwa wachezaji wetu wote na sasa zoezi linalofuata ni kuanza mazoezi kesho (leo) Ijumaa kwenye Uwanja wa KMC na baada ya hapo ratiba nyingine zitatolewa,” kilisema chanzo hicho na kuongeza;

“Maandalizi yatakuwa chini ya benchi la ufundi jipya na imani yetu ni kuona wachezaji wote wanaanza programu isipokuwa wachezaji walipo kwenye kikosi cha timu ya taifa kujiandaa na michuano ya CHAN.”

Chanzo hicho kilisema taarifa juu ya kuanza maandalizi zimetolewa kwa wachezaji wote tangu siku ya kwanza walipoanza vipimo hivyo matarajio ni kuona wachezaji wote wanafika kwa wakati kuanza program.

“Siwezi kuweka wazi ni wachezaji gani wa kigeni ambao tayari wamewasili hadi sasa ninachoweza kusema wachezaji wote wanatakiwa kuanza programu kesho (leo) chini ya benchi jipya la ufundi.”

Mwanaspoti linafahamu kwa mujibu wa ratiba hiyo basi kikosi kitakuwa na siku 13 za maandalizi, kwani timu hiyi inatakiwa kuondoka nchini kuifuata Rayon Sport kwa mchezo wa kirafiki wa kimataifa unaotarajia kuchezwa Agosti 15 mwaka huu.

Yanga iliyotwaa ubingwa wa Ligi Kuu na Kombe la F kwa misimu minne mfululizo na hadi sasa imedaiwa kuwasajili nyota wapya kama watano, akiwamo Celestin Ecua, Bella Mousa Konte, Mohamed Doumbia mbali na kuwaongeza mikataba Israel Mwenda, Mudathir Yahya, Pacome Zouzoua na Aziz Andambwile.