ALIYEKUWA kocha wa Tanzania Prisons, Abdallah Mohamed ‘Bares’ amesema kuna la kujifunza katika Fainali za Ubingwa kwa Mataifa ya Afrika (CHAN) 2024 kimbinu, ufundi na uzalendo kupitia mechi mbalimbali zitakazochezwa.
Alitoa wito kwa makocha na wachezaji kutenga muda wa kuifuatilia michuano hiyo, ili kupata kitu cha kujifunza kutoka katika mataifa mbalinbali yaliyopo nchini.
“Michuano hiyo inamgusa kila Mtanzania kwa aina yake, inatangaza nchi na vivutio vyake, inatoa fursa kwa wafanyabiashara kukuza uchumi wao, makocha na wachezaji kuona mbinu za wenzetu zitakazotuongezea kitu katika soka letu,” alisema Bares.
Mechi ya ufunguzi ilifanyika jana Jumamosi kati ya mwenyeji Tanzania dhidi ya Burkina Faso, jambo ambalo Bares alisema endapo kila Mtanzania akiisapoti Stars kwa nafasi yake, anaamini itafika mbali na huenda ikachukua taji la Chan.
“Kwa mara ya kwanza Chan kufanyika Tanzania, hivyo tuna kila sababu ya kulipambania kombe hilo, kocha Hemed Morocco ni mzuri wa mbinu na wachezaji kawaandaa kwa kuipambania bendera ya Tanzania,” alisema.
Mbali na hilo, alizungumzia kwa nini hakujiunga na Tanzania Prisons aliyokuwa anahusishwa nayo.
“Ni kweli ilikuwa nikaifundishe timu hiyo msimu ujao, ila tulishindwana kwa maslahi.
“Timu zinakuja na kuondoka, wakati sahihi ukifika wa kusaini nitafanya hivyo, kwa sasa haijapangwa na Mungu niende timu gani,” alisema.