Dar es Salaam. Licha ya ongezeko la shughuli za ujenzi wa miundombinu jijini, ikiwemo barabara, biashara za aina mbalimbali, zikiwemo za vyakula zinaendelea kufanyika pembezoni mwa maeneo yenye vumbi jingi, hali inayoweka afya za walaji hatarini.
Vumbi linalopeperushwa hewani huambatana na chembechembe za uchafu na vimelea vya magonjwa, hali inayotajwa na wataalamu wa afya kuwa chanzo kikuu cha magonjwa ya mfumo wa chakula na kupumua kama kipindupindu, homa ya matumbo, pumu na kikohozi sugu.
Hii ni kwa kuwa vumbi linaweza kubeba kinyesi cha binadamu au wanyama kilichokauka na linapovutwa na wapishi au wateja wao linaweza kusababisha magonjwa ya mapafu na mfumo wa hewa kama kikohozi, pumu na kusinyaa kwa mapafu.
Licha ya hatari iliyopo kutokana na vumbi, katika mitaa mingi jijini Dar es Salaam kwa sasa ujenzi wa barabara unaendelea, lakini pembezoni biashara za vyakula nazo zinafanyika.
Katika mazingira hayo, kipindi cha sasa cha upepo mkali, vumbi hutimka na kuathiri pakubwa biashara hizo.
Miongoni mwa maeneo yanayoathirika ni Buguruni katika Barabara ya Mandela, Barabara ya Bagamoyo na penginepo.
Mbali na vyakula vinavyopikwa, zipo pia biadhara za na matunda ambayo baadhi humenywa na kuachwa wazi pasipo kufunikwa.
Hali hiyo isipodhibitiwa kwa kuzuia vumbi na majimaji visifike kwenye vyakula, magonjwa ya mfumo wa chakula na hewa yanaweza kuwasumbua walaji, kwa mujibu wa wataalamu wa afya.
Hata hivyo, akizungumza na Mwananchi, mfanyabiashara wa chapati katika eneo la Buguruni, Ernest Loitai amesema licha ya uwepo wa vumbi wakati wa kuziandaa, anaamini baada ya kuzichoma, hata kama kutakuwa na vijidudu vya vimelea vya magonjwa, vitakufa.
“Ikiwa ya moto sidhani kama bakteria wanaweza kukaa, najitahidi kuhakikisha kile kinachofika kwa mteja kinakuwa safi. Ugumu wa biashara ya chapati huwezi kupika nyumbani, wengine wakija wanataka iliyotoka motoni muda huo,” amesema.
Kwa upande wake, Faudhia Hassan, muuzaji wa chakula anasema amekuwa akihakikisha anakipika katika hali ya usafi nyumbani, kabla ya kwenda kukiuza katika eneo hilo la Buguruni.
“Ni vile tu eneo hili kwa sasa linajengwa ndiyo maana kuna vumbi jingi, zamani kulikuwa shwari. Hili vumbi ni la siku za hivi karibuni ila vyakula tuhakikisha vimefunikwa muda wote,” amesema Faudhia.
Amesema yeye na wachuuzi wenzake vumbi limekuwa likiwasababishia maradhi ya mara kwa mara ya mafua na kikohozi.
“Sisi wenyewe tuna hali ngumu hivi sasa, kukohoa, mafua ni sehemu ya maisha yetu kwa kipindi hiki, lakini hatuwezi kulala kwa sababu hapa ndiyo sehemu ambayo kodi zinapatikana, watoto wanaenda shule na kula,” amesema Faudhia.
Wafanyabiashara wakieleza hayo, baadhi ya wateja wanasema hali ya vumbi imesababisha wabadili utaratibu wao wa ulaji, wengine wakilazimika kwenda kula nyumbani.
“Tofauti na zamani unakaa hapa unakula unaenda nyumbani kamili. Hivi sasa kuna vumbi sana, huwezi kula kwa raha maana hapa magari muda wote yanapita huwezi kusema muda huu ni angalau labda usiku,” amesema Richard Mwendapole, mkazi wa Buguruni kwa Mnyamani.
“Sasa sehemu hii pia ndiyo uhakika na ukizoea kula chakula cha mtu fulani, kula sehemu nyingine ni vigumu, ndiyo maana tunalazimika kubadilisha namna ya kupata chakula.
Daktari katika Hospitali ya Wilaya ya Bagamoyo, Medard Ndayanse amesema mara nyingi mtu hushauriwa kutokula chakula katika eneo lenye vumbi kutokana na athari anazoweza kupata kiafya.
Hali hiyo amesema inatokana na vumbi hubeba bakteria wanaoweza kusababisha maambukizi ya magonjwa mbalimbali ikiwemo homa ya matumbo na magonjwa ya kuhara na tumbo.
“Kama ni vigumu kula katika eneo lisilokuwa na vumbi, basi mhusika akae sehemu yenye vumbi kidogo, japokuwa inashauriwa mtu ale chakula sehemu tulivu isiyokuwa na vumbi kabisa,” amesema Dk Medard.
Kwa upande wake, Dk Ernest Winchislaus, mtaalamu mwingine wa magonjwa ya binadamu, amesema baadhi ya vyakula vinavyouzwa pembezoni mwa barabara huwa viko katika mazingira yasiyo safi na salama.
Hiyo ni kwa sababu vumbi au majimaji yanayoweza kurushwa na magari hubeba vimelea vya magonjwa yanayoweza kuathiri mfumo wa chakula wa mtu na kusababisha magonjwa kama kuharisha, kipindupindu na homa ya matumbo.
“Vyakula hivi si salama sana kwa ajili ya kuliwa, ni vyema watu kuepuka kununua hasa vile ambavyo vimeshapikwa na kuuzwa pembezoni mwa barabara. Kama ni matunda anunue aende nyumbani kuosha ili uwe salama,” amesema.
Kwa vyakula amesema ni vyema mtu akala kikiwa bado cha moto kwani uwezekano wa bakteria kuwa hai unakuwa ni mdogo tofauti na kikiwa cha baridi.
“Lakini kabla ya kula chochote ni vyema kuhakikisha unanawa mikono vizuri kwa kutumia maji tiririka na sabuni hii itakuondoa katika hatari ya kupata maambukizi hayo,” amesema.
Mtaalamu wa Lishe, Dk Daudi Gambo amesema katika uandaaji wa chakula zipo kanuni ambazo zinapaswa kuzingatiwa, ikiwemo mazingira safi na namna muandaaji anavyopaswa kuvaa wakati anapika.
“Hivyo ulaji wa chakula hapo ni hatarishi kwani vyakula vinavyouzwa pembeni ya barabara ni kinyume cha sheria na upo uwezekano mkubwa wa kuchafuliwa na bakteria hatarishi,” amesema.
Amesema hali hiyo inasababishwa na watu na magari yanayopita kutimua vumbi, hivyo uwezekano wa vyakula kupata vimelea vya magonjwa ni mkubwa hata kama kinatoka motoni.
“Hata kama kikitoka motoni sasa hivi je, kimeandaliwa katika mazingira gani kwa ajili ya kuliwa, je, watu wananawa na sabuni? vyombo vinavyooshwa, kuna maeneo wanaosha sahani na maji waliyotumia si masafi, hata muoshaji hakaushi sahani wakati ambao maji aliyotumia yamechafuka,” amesema.
Ili kuepukana na hali hiyo, wataalamu wanashauri watu kula chakula katika maeneo safi na kilichoandaliwa katika hali ya usafi.