TOFAUTI na ilivyozoeleka katika mechi nyingi za ndani, ambapo mageti ya viwanja hufunguliwa mapema ili kuwapa mashabiki nafasi ya kuingia mapema, hali imekuwa tofauti kwenye ufunguzi wa mashindano ya CHAN 2024.
Uwanja wa Benjamin Mkapa ambao utatumika kwa ufunguzi wa mashindano hayo ulinzi ni mkubwa huku mashabiki wakizuiwa kuingia mapema kama ilivyo kawaida.
Mashindano hayo ya CHAN ambayo mwaka huu yanafanyika kwa mara ya kwanza katika ukanda wa Afrika Mashariki yanaonekana kuwa na hamasa uwanjani hapo.
Katika viunga vya Uwanja wa Mkapa ambako mechi ya ufunguzi inatarajiwa kuchezwa mashabiki wamekuwa wakimiminika kwa wingi huku idadi ikiongezeka kadri muda unavyosogea.
Hali hiyo imeleta hamu kubwa ya kutaka kushuhudia mechi ya kwanza ya mashindano hayo, ambapo Taifa Stars ya Tanzania itakuwa na kibarua kizito. Hata hivyo, uwanja huo umeendelea kuwa na ukaguzi ambapo ni watu wachache tu wanaoruhusiwa kuingia na kutoka.
Walioruhusiwa ni wale wanaobeba vitambulisho maalumu vya uratibu, wanahabari na maofisa wa usalama. Tanzania iliyo kundi B inatarajiwa kushuka dimbani saa 2:00 usiku dhidi ya Burkina Faso.