Chanzo makosa ya usalama barabarani kupaa Zanzibar

Unguja. Wakati makosa makubwa ya jinai yakipungua kwa kipindi cha Januari hadi Juni, 2025 yale ya usalama barabarani yameongezeka kwa asilimia 70.4 katika kipindi hicho, hali inayowashtua wadau wakishauri hatua za kuchuua.

Akitoa taarifa kwa waandishi wa habari leo Agosti 2, 2025, Kamishna wa Polisi Zanzibar, Kombo Khamis Kombo amesema makosa ya usalama barabarani yameongezeka na kufikia 28,740 ikilinganishwa na 16,870 yaliyoripotiwa kipindi kama hicho mwaka 2024.

“Hili ni ongezeko la makosa 11,870 sawa na asilimia 70.4, utaona namna ambavyo kuna changamoto nyingi za barabarani, sisi Jeshi la Polisi bado tuna kazi kubwa ya kufanya,” amesema.

Katika makosa ya usalama barabarani waliopoteza maisha katika kipindi hicho ni watu 96, huku waliojeruhiwa wakiwa 150. Mikoa inayoongoza kwa makosa hayo ni Kaskazini Unguja na Mjini Magharibi.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri na Usalama Barabarani, Haji Ali Zubeir akizungumza na Mwananchi kuhusu ongezeko la makosa hayo amesema ni uzembe unaofanywa na madereva wasiozingatia sheria ya usalama barabarani.

Hata hivyo, amesema hatua kali zinaendelea kuchukuliwa kwa madereva wanaosababisha ajali na makosa mengine barabarani, ikiwamo kuwanyang’anya leseni na hatua zingine kwa mujibu wa Sheria ya Makosa Barabarani namba saba ya mwaka 2003.

Amesema ndani ya Juni pekee wamewafungia leseni moja kwa moja madereva 187. Kati ya hao waendesha pikipiki ni 162 na madereva wa magari 25.

“Hatua zinaendelea kuchukuliwa kwa mujibu wa sheria, adhabu ya makosa haya ni kufungia leseni, kutozwa faini au vyote kwa pamoja. Sasa kwa mwezi mmoja tu tumewafungia leseni moja kwa moja madereva hao lakini wapo wengine wanachukuliwa hatua za faini na vifungo,” amesema.

Aisha Abdallah Haji, mdau wa usafirishaji amedai trafiki huangalia zaidi magari ya abiria yanayojaza lakini hawashughuliki na mambo mengine.

“Hili ni changamoto, mara nyingi askari wanaangalia kujaza abiria, lakini hawashughulikii mambo mengine ukiwemo ubovu wa magari, hivyo kuchangia kuongezeka kwa ajali,” amesema.

Ussi Abubakar Said amesema madereva hawazingatii alama za barabarani kwa watembea kwa miguu, huku zingine zikiwa zimefutika bila kurejeshwa kwa kipindi kirefu.

Wakati wa Mkutano wa 19 wa Baraza la Wawakilishi, Naibu Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Nadir Abdulatif, akijibu hoja za wajumbe alieleza sababu za kutowekwa alama za barabarani hususani za watembea kwa miguu akieleza ni kutokana na barabara zinazoendelea kujengwa.

Zanzibar ipo katika ujenzi wa barabara za mjini kilomita 100.9 na kilomita 275 barabara za vijijini, huku zaidi ya mtandao wa kilomita 800 zikijengwa Unguja na Pemba.

Hata hivyo, alisema kwa baadhi ya maeneo wanaweka alama licha ya uhalisia kuwa maeneo mengi hususani ya vivuko vya waenda kwa miguu hayana alama za pundamilia.

Kamishna Kombo amesema makosa 1,195 ya jinai yameripotiwa kati ya Januari hadi Juni 2025 ikilinganishwa na makosa 1,652 yaliyoripotiwa kipindi kama hicho mwaka 2024 ikiwa ni upungufu wa makosa 457 sawa na asilimia 27.7.

Amesema makosa 409 dhidi ya binadamu yameripotiwa ikilinganishwa na makosa 611 ya kipindi kama hicho mwaka jana sawa na upungufu wa makosa 202 ikiwa ni asilimia 33.1. Makosa hayo ni ya mauaji, kubaka na kulawiti.

Kwa makosa ya kubaka amesema yameripotiwa 338, ikilinganishwa na 468 ya kipindi kama hicho sawa na asilimia 27.8. Vyanzo vya makosa hayo amesema ni mmomonyoko wa maadili.

Kati ya makosa 338 ya kubaka, amesema makosa 222 wahusika ni wasichana na wavulana au wapenzi waliokubaliana kwa ridhaa yao lakini kutokana na matakwa ya kisheria msichana mwenye miaka 18 hutambulika bado ni mtoto, hivyo makosa halisi ya kubaka yapo 116.

“Katika hili kuna changamoto ambayo hujitokeza mbele ya mahakama katika kutoa ushahidi baadhi ya mashahidi ambao ni wasichana hukataa kosa la kubakwa na kuendelea kumtetea mtuhumiwa kuwa hakumbaka, bali wao ni wapenzi na walifanya kwa hiari na wakati mwingine hukana mbele ya Mahakama kutomfahamu mtuhumiwa,” amesema.

Kuhusu kulawiti amesema yameripotiwa makosa 42 ikilinganishwa na 108 ya kipindi kama hicho mwaka 2024 sawa na asilimia 61.

Kuhusu makosa ya kuwania mali, Kamishana Kombo amesema yameripotiwa 755 ikilinganishwa na makosa 935 yaliyoripotiwa kipindi kama hicho mwaka 2024 ikiwa ni sawa na upungufu wa asilimia 19.2.

Makosa ya wizi wa pikipiki na mifugo yameongezeka, ya wizi wa mifugo yakiwa 195 ikilinganishwa na 177 ya mwaka jana sawa na ongezeko la asilimia 10.2

Makosa ya uvunjaji, yameripotiwa 283 ikilinganishwa na 439 sawa na asilimia 35.5.

Amesema katika kipindi hicho kesi 317 zimepata mafanikio mahakamani, kesi 182 zimefutwa, 68 zimefutwa katika vituo vya polisi, 38 zipo ofisi ya Mkurugenzi wa Mashataka, 21 zimehamishiwa Tume ya Kupambana na Kuzuia Dawa za Kulevya Zanzibar, 210 zipo chini ya upelelezi na 359 zinaendelea kusikilizwa mahakamani kwa hatua mbalimbali.