KIUNGO mshambuliaji wa timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, Feisal Salum ‘Fei Toto’ amesema ni fahari kwa kikosi hicho kuanza vyema fainali za Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ligi za Ndani (CHAN), baada ya ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Burkina Faso.
Stars imepata ushindi huo wa mechi ya kwanza ya ufunguzi wa michuano hiyo kwa mabao yaliyofungwa na Abdul Suleiman ‘Sopu’ kwa penalti na Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ aliyetupia kwa kichwa.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya mechi hiyo, Feisal amesema ushindi huo ni mzuri na unawafanya Watanzania wote kufurahia matokeo hayo.
“Lengo letu ni kuhakikisha tunashinda kila mechi kwa sababu michuano hii inafanyika nyumbani na sisi tunahitaji kuonyesha uimara katika kila hatua tunayofuata,” amesema.
Feisal amechaguliwa kuwa mchezaji bora wa mechi hiyo, ambapo kwa sasa Stars inaongoza kundi B baada ya kufikisha pointi tatu, huku Burkina Faso ikiburuza mkia.