Hali ilivyo Uwanja wa Mkapa

MIONGONI mwa kauli alizozitoa kipa wa timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ Aishi Manula aliyetoa wito kwa Watanzania kujitokeza kwa wingi ili kuisapoti katika mechi ya ufunguzi wa Kombe la Mataifa Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN) dhidi ya Burkina Faso, alisema: “Tupo katika ardhi ya nyumbani, Watanzania waje ili tujisikie nguvu ya kupambana.”

Taifa Stars inacheza dhidi ya Burkina Faso mechi itayopigwa kuanzia saa 2:00 usiku kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, lakini kwa sasa kuna mambo kadhaa yanayoendelea yakishabihiana na wito wa Manula, ikiwamo namna Watanzania walivyoanza kuitikia.

MASHABIKI UWANJANI
Watanzania wameitikia wito wa kujitokeza kwa wingi kufika Uwanja wa Benjamin Mkapa, kuisapoti timu ya taifa ya Tanzania Taifa Stars itakayokuwa na mechi dhidi ya Burkina Faso.

Nyomi ya watu imejaa nje ya uwanja ikisubiri saa 2:00 ambapo mechi hiyo itakayopigwa, huku wengine wakiwa sehemu ya vinywaji na chakula wakipata huduma.

Mbali na hao, wapo ambao wanatembea, baadhi wakiwa wamejichora rangi za bendera ya Tanzania, wengine wakiwa wamebeba vikapu vilivyoandika ujazo wa mabao wakiamini bendera ya taifa inakwenda kupeperushwa vyema, huku wakisubiri ruhusa maalumu ya kufunguliwa mageti ili waingie uwanjani.

Taarifa zinadai mageti hayo yatafunguliwa saa tatu kabla ya mchezo huo kuanza, ambapo kwa sasa hakuna anayesogelea ukuta wa uwanja kutokana na ulinzi mkali uliopo.

BIASHARA
Kupitia michuano ya CHAN baadhi ya Watanzania wamenufaika na kufanya biashara za vyakula, vinywaji, matunda na bidhaa mbalimbali kandokando mwa Uwanja wa Mkapa.

Mmoja wa mamalishe aliyejitambulisha kwa jina la Aisha amesema:”Biashara inaenda vizuri naamini hadi michuano iishe nitakuwa nimenufaika na kujipatia kipato.”

Hata hivyo, tofauti ilivyozoweleka kwa mashabiki wa Dar, mara hii vyakula na vinywaji vyote vinauzwa nje ya uwanja kwenye mabanda maalumu ambao yametengenezwa jirani na Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Mabanda hayo ambayo yamenakshiwa urembo maalumu wa maandishi ya fainali hizo ndiyo yanatumiwa na wafanyabiashara wote wa vyakula, vinywaji na hata wale wanaouza jezi na vifaa vingine na kwenye kila banda kuna walinzi maalumu maarufu kwa jina la mgambo ambao wana kazi ya kuhakikisha maeneo hayo amani inatawala.


Tofauti na ilivyozoeleka ikichezwa mechi ya Dabi ya Kariakoo kati ya Simba na Yanga ambapo kunakuwa na mipaka ya kukaa mashabiki wakisubiri kuingia uwanjani, awamu hii wamewekwa mbali zaidi na geti kubwa la kuingilia uwanjani.

Uzio wa kuwatenganisha mashabiki hao na geti la kuingilia uwanjani umesogezwa nyuma zaidi pamoja na sehemu za maegesho ya usafiri – kwa maana ya magari na bodaboda vyote vikiwa mbali.


Pamoja na hayo ulinzi umeimarishwa kukiwa na askari ndani ya uzio na wengine nje, huku hali ya utulivu ikiwa imetawala na stori za hapa na pale za mashabiki wanaosubiri kuona Stars itafanya kitu gani katika mechi ya ufunguzi dhidi ya Burkina Faso.