Mwenyekiti
wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji wa Mahakama ya Rufani Jacobs
Mwambegele akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutanio wa Tume na Waandishi wa
Habari kuhusu uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025. Kikao hicho cha siku moja
kilifanyika jijini Dar es Salaam leo Agosti 02 , 2025.
::::::::::
Na Waandishi Wetu, Dar es
Salaam
Waandishi wa habari nchini
wametakiwa kutumia taaluma yao kuhamasisha na kuelimisha wananchi kujitokeza
kwa wingi kupiga kura ifikapo tarehe 29 Oktoba, 2025.
Wito huo umetolewa na
Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji wa Mahakama ya Rufaa Jacobs Mwambegele,
wakati akifungua Mkutano wa Kitaifa kati ya Tume na Waandishi wa Habari kuhusu
Uchaguzi Mkuu, uliofanyika tarehe 2 Agosti, 2025 katika ukumbi wa Mlimani City,
jijini Dar es Salaam.
Jaji Mwambegele amesema
vyombo vya habari vina mchango mkubwa katika kuhakikisha wananchi wanashiriki
kikamilifu kwenye uchaguzi mkuu kwa kuwapatia taarifa sahihi na kwa wakati
kuhusu masuala mbalimbali ya uchaguzi.
Ameeleza kuwa waandishi wa
habari wana wajibu mkubwa wa kutumia taaluma yao kuwaelimisha wananchi
waliojiandikisha kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, ili waweze kujitokeza
kwa wingi kushiriki zoezi la kupiga kura.
Kwa upande wake,
Mkurugenzi wa Uchaguzi Kailima Ramadhani
amewakumbusha wanahabari wajibu wao wa kuhakikisha vyama vya siasa na wagombea
wanapata nafasi ya kufikisha ujumbe wao kwa wapiga kura katika kipindi cha
kampeni.
Aidha, Kailima amewataka
wanahabari kutoa taarifa sahihi kwa umma na kuepuka kusambaza taarifa potofu
katika hatua zote za mchakato wa uchaguzi, huku akisisitiza umuhimu wa
kuzingatia sheria na maadili ya taaluma ya habari.
Katika hatua nyingine amewaasa kuepuka kuchapisha au kurusha habari
zinazoweza kuwavunja moyo wananchi na kuwafanya waone kama hakuna umuhimu wa
kushiriki katika uchaguzi, iwe ni kama wapiga kura au wagombea.
Mkutano kati ya Tume na
Waandishi wa Habari ni sehemu ya mfululizo wa mikutano ya wadau mbalimbali
ambayo Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi imekuwa ikiitisha katika maandalizi ya
kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025.
Mikutano hiyo ilianza
tarehe 27 Julai 2025 kwa kukutana na Viongozi wa Vyama vya Siasa, ikafuatiwa na
mkutano na Wawakilishi wa Asasi Zisizo za Kiserikali kisha Wawakilishi wa
Wanawake, Vijana na Watu Wenye Ulemavu, pamoja na Wahariri wa Vyombo vya Habari.
Mfululizo huu wa mikutano
unatarajiwa kuhitimishwa tarehe 4 Agosti 2025, baada ya mkutano na Waandaji wa
Maudhui Mtandaoni, utakaofuatiwa na mafunzo kwa Wahariri na Waandishi wa
Habari.
Mkurugenzi
wa Uchaguzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Ndg. Ramadhani Kailima
akizungumza wakati wa kuwasilisha mada katika mkutano wa Tume na Waandishi wa
Habari kuhusu uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025. Kikao hicho cha siku moja
kilifanyika jijini Dar es Salaam leo Agosti 02 , 2025.