Dodoma. Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) imesema ujenzi wa jengo jipya jijini Dodoma ambalo linagharimu Sh8 bilioni ni sehemu ya mikakati ya Serikali kuboresha miundombinu ya utafiti na ubunifu nchini.
Mwenyekiti wa COSTECH, Profesa John Kondolo ameyasema hayo jana Ijumaa Agosti 1 2025 wakati alipokuwa akikagua jengo hilo ambalo litakuwa ni makao makuu ya tume hiyo.
Profesa Kondolo amesema wamejiridhisha na maendeleo ya ujenzi ambao umeendana na masharti ya mkataba yanayotaka kukamilika ifikapo Machi 2026.
“Jengo hili litakapokamilika litakabidhiwa kwa COSTECH kama msimamizi mkuu wa masuala ya utafiti, maendeleo ya sayansi, teknolojia na ubunifu nchini,”amesema.
Amesema kwa kiwango na ubora wa kazi waliyoshuhusia, vinawapa matumaini kuwa litakuwa na hadhi ya kitaifa na kimataifa katika kuendeleza sekta za sayansi na teknolojia.
Mkurugenzi Mkuu wa COSTECH, Dk Amos Nungu amesema mradi huo unatekelezwa kwa kutumia fedha za Serikali takriban Sh8 bilioni ukiwa ni sehemu ya mikakati ya Serikali kuboresha miundombinu ya utafiti na ubunifu nchini.
Dk Nungu amefafanua kuwa jengo hilo litakuwa na kumbi za bunifu, kumbi za mikutano ya wanasayansi, na maabara za kisasa zitakazowezesha watafiti kufanya kazi kwa ufanisi zaidi.
“Tunategemea pia na nafasi maalum kwa ajili ya wabunifu kupata huduma za atamizi (incubation) ili kukuza mawazo na ubunifu mpya,baada ya makao makuu kuhamia Dodoma, nafasi iliyokuwa ikitumika Dar es Salaam itatumika kikamilifu kwa ajili ya huduma hizo,” amesema Dk Nungu.
Aidha, Dk Nungu amesema kukamilika kwa jengo hilo kutarahisisha uratibu wa shughuli za kitaifa za utafiti na teknolojia kutokana na uwepo wa miundombinu ya kisasa na mazingira bora ya kazi kwa wataalamu na wabunifu.
Kwa upande wake, Msanifu Majengo wa mradi huo, Benedict Martin amesema usanifu wa jengo hilo umezingatia vigezo vya kisayansi na kiteknolojia kwa kuhakikisha linaendana na mahitaji ya utafiti na uvumbuzi wa kisasa.
Martin amesema usanifu huo umejumuisha ofisi za kisasa, kumbi za mafunzo, maeneo ya maonyesho ya teknolojia, na mifumo ya kidigitali itakayorahisisha mawasiliano ya kitaifa na kimataifa kwa COSTECH.
Kukamilika kwa makao hayo makuu kunatarajiwa kuimarisha zaidi nafasi ya Tanzania katika utafiti na maendeleo ya kisayansi, ikileta urahisi kwa wanasayansi, wabunifu na sekta binafsi kushirikiana katika kukuza teknolojia na ubunifu nchini.
Profesa Kondolo alihitimisha kwa kusema kuwa Serikali inaendelea kuwekeza kwenye miundombinu ya sayansi na teknolojia kwa lengo la kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha uvumbuzi Afrika Mashariki na hatimaye kufanikisha uchumi wa kidigitali.