Hapa Uwanja wa Benjamin Mkapa, uzalendo umewekwa mbele kwa mashabiki wengi kuvaa jezi za timu ya taifa badala ya zile za klabu.
Tanzania kupitia Taifa Stars, leo itacheza mchezo wa ufunguzi wa Fainali za Mataifa Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN), itakapokutana na Burkina Faso, mechi itakayoanza saa 2:00 usiku.
Nje ya uwanja wa Mkapa jezi nyingi zilizovaliwa ni zile za timu ya taifa ambazo ndizo mashabiki wengi wamezitinga.
Ukiacha wale waliozivaa pia wapo wengine wameendelea kuzinunua ili wafanane na wenzao wanaosubiri mchezo huo.
Jezi za Stars zinauzwa kuanzia Sh30,000 na kuendelea, lakini bado mashabiki wanazinunua kwa wingi.
Hata hivyo, wapo wachache wameendelea kubaki na jezi za klabu zao wakionekana na jezi za Simba, Yanga na hata Mtibwa Sugar.
Kwa mujibu wa wauzaji wa jezi zile za klabu haziuziki kwa sasa ambapo hata wale wanaoulizia bei wamekuwa wanaulizia zile za timu ya taifa.