Namungo na Dodoma Jiji zimeingia vitani kuisaka saini ya aliyekuwa kocha mkuu wa Tanzania Prisons, Aman Josiah, lakini inadaiwa itakayokuwa na mkwanja mnene inaweza ikafanikisha dili hilo kwani kwa sasa kocha huyo hana timu.
Chanzo cha ndani kutoka Namungo kilisema uongozi umeshawishika kutaka huduma ya Josiah kutokana na kile alichokifanya akiwa na Prisons msimu uliyopita, hivyo wanaamini atakuwa chachu ya timu kufanya vizuri endapo wakifanikiwa kumpata.
“Josiah alikwenda kuifundisha Prisons ikiwa na hali mbaya tena alitokea timu ya Geita Gold ya Championship, lakini bado akafanya makubwa, ndiyo maana tunaipambania huduma yake ili tuwe naye kwa msimu ujao,” kilisema chanzo hicho na kuongeza;
“Bado mazungumzo yanaendelea ya kimasilahi ili kila mtu aweze kunufaika kwa upande wake, endapo tukifanikisha hilo tutawajulisha.”
Kama Namungo itafanikiwa kuinasa saini ya Josiah atakwenda kuzipa pengo la kocha Juma Mgunda iliyeachana naye baada ya msimu uliyopita kuongoza timu hiyo kumaliza nafasi ya tisa katika mechi 30, ilishinda tisa, sare nane, ilifungwa 13 ilivuna pointi 35.
Chanzo kutoka Dodoma kilisema: “Kocha Josiah anafundisha soka la kisasa na ana uwezo wa kuibadilisha timu kama alivyofanya Prisons ambayo msimu uliyopita ilianza vibaya, lakini akaisaidia kuibakiza kwa mechi za mwisho kucheza mtoano (playoffs).”
Alipotafutwa kocha Josiah ili kuthibitisha hilo alisema: “Mojawapo ya timu ulizozitaja mazungumzo yanaendelea nikifikia nao mwafaka, nitajiunga nao kwa ajili ya msimu ujao, ila kwa sasa naendelea na mapumziko ya kuingiza vitu vipya kichwani kabla ya kuanza kwa majukumu.”