YANGA imeshamalizana na kiungo mmoja wa kigeni, Mohammed Doumbia na mshambuliaji Celestin Ecua na kilichobaki kwa sasa ni kuwatambulisha tu, lakini kuna kocha mmoja Mfaransa aliyekuwa akifuatilia usajili wa timu hiyo ametoa kauli ambayo inaweza kuwa kama salamu kwa timu pinzani.
Kocha huyo aliyekuwa hatua ya mwisho kutua Jangwani, kabla ya dili hilo kufa na kuletewa Mfaransa mwenzake kijana, Romain Folz, amesema kwa mziki uliosajiliwa Yanga ni wazi wapinzani wanapaswa kujihadhari mapema kabla ya kukutana na kikosi hicho kwa msimu mpya wa mashindano.
Kocha aliyetoa tahadhari hiyo ni kocha wa ASEC Mimosas ya Ivory Coast, Julien Chevailer ambaye dili lake la kutua Yanga lilikwama mwishoni baada ya mabosi wa klabu yake ya Asec kuamua kumbakisha baada ya awali kumaliza mkataba aliokuwa nao.
Chevailer aliyekuwa na mpango ya kushuka sambamba na Ecua aliyekuwa akiitumikia timu hiyo ya ASEC, aliliambia Mwanaspoti kwa njia ya simu kutoka Ufaransa, hatua ya Ecua kumalizana na Yanga kisha kuungana na viungo wenye kasi, itazisumbua safu nyingi za mabeki kwa wapinzani wao.
Chevalier aliyefanya kazi na Ecua kwa miezi sita akiwa na ASEC Mimosas iliyokuwa inammiliki kwa mkopo kutoka Zoman FC, alisema mabeki wengi hawapendi kukabiliana na viungo au washambuliaji wenye kasi kama aliyonayo straika huyo aliyemaliza kama MVP wa Ligue 1 na Pacome Zouzoua.
Kocha huyo alisema safu ya Yanga itakuwa na hatari kwa wapinzani, kwani wachezaji hao wawili anawajua namna wanavyoweza kuinua timu yao hata kama ipo nyuma.
“Nimefanya kazi na wote Ecua na Zouzoua (Pacome), nadhani Yanga wanatengeneza safu katili ya kiungo na washambuliaji, itasumbua sana wapinzani,” alisema Chevalier na kuongeza;
“Nionyeshe mabeki wawili wanaopenda kukabiliana na washambuliaji au viungo wenye kasi, sio rahisi kwao hawapendi nawajua wanapenda kukutana na wachezaji ambao hawana kasi.
“Unamwona Ecua, anaweza kushuka chini kusaidia na kukimbia katika nafasi na kutengeneza madhara makubwa, hivyo hivyo Zouzoua bado kuna wengine pale nawajua nao wana kasi pia.
Kocha huyo anayesifiwa kwa kupenda soka la vijana na kuifanya Asec kuwa kama chuo cha kuzalisha mastaa wanaonunuliwa na klabu mbalimbali ikiwamo kutoka Tanzania, aliongeza kwa kusema; “Kwangu usajili uliofanywa na Yanga ni mzuri, naamini watafurahia sana kwa kuwa wamepata mchezaji mwenye njaa ya mafanikio na anayejituma sana uwanjani,” alisema kocha Chevaliwer.
Mshambuliaji huyo aliyefunga mabao 15 na asisti 12 katika Ligi ya Ivory Coast, tayari ameshatua jiji Dar ili kukamilisha usajili na kujiunga na timu kabla ya kujiandaa kusafiri kwenda Rwanda kwa mechi ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya Rayon Sports itakayopigwa Agosti 15 kisha kutimkia Sauzi.
Lakini, Ecua hajatua pekee yake kwani Mwanaspoti linafahamu Yanga imemshusha pia kiungo mshambuliaji Mohamed Doumbia.
Taarifa za ndani liliambia Mwanaspoti Yanga kwa sasa imekuja na mpango wa kuwapa mastaa wake wapya mikataba ya miaka mitatu.
“Ecua amesaini mkataba wa miaka mitatu kuitumikia Yanga ambapo wakati wowote, usajili huo utawekwa hadharani akiwa staa wa pili wa kigeni, akitanguliwa na Lassine Koume na Balla Mousa Konte waliotambulishwa mapema sambamba na straika mwingine mkali, Andy Boyeli.
Yanga imeanza kambi ya mazoezi jana Agosti 1, 2025 kabla ya Agosti 13 itasafiri kwenda Rwanda kisha baada ya hapo itahamia Afrika Kusini badala ya Misri kama ilivyokuwa imepanga kutokana na watani wao, Simba kuwahi huko mapema katika jiji la Ismailia.