UTARATIBU wa kuingia Uwanja wa Benjamin Mkapa unaotarajiwa kupigwa mechi ya ufunguzi wa michuano ya Chan kati ya Tanzania na Burki Faso umezingatia ustaarabu.
Kabla ya mageti kufunguliwa nyomi ya watu ilijaa nje ya uwanja, wakisubiri kuingia ili kushuhudia mechi hiyo inayotarajiwa kuchezwa kuanzia saa 2:00 usiku, lakini baada ya kuruhusiwa kila kitu kinakwenda bila vurugu.
Kwa sasa mashabiki ni wachache na hakuna foleni ya kuingia ndani, huku askari wakionekana kuimarisha ulinzi kila sehemu ili kuhakikisha hakuna kinachoharibika.
Tofauti na inavyokuwa katika mechi za Ligi Kuu Bara ambapo mashabiki wakipungua baadhi yao, wanaokuwa hawana tiketi wanasogea karibu na geti la kuingilia lakini kwa sasa wameendelea kusalia nje ya eneo la uzio lililowekwa mbali.
Baadhi ya mashabiki waliopo nje ya uwanjani wamezungumza na Mwanaspoti kipi kimewasibu kutoingia ndani.
Issa Jacob amesema: “Tiketi za mzunguko tulitangaziwa Sh2,000, lakini maeneo niliyoenda wanauza Sh5,000, hivyo nitasalia hapa kwa muda kisha narudi nyumbani.”
Prisca Ashley amesema:”Japokuwa sitaingia ndani kutokana na kukosa tiketi sina pesa, lakini kitendo cha kuwepo nje ya uwanja ni uzalendo, nimeisapoti Stars kwa aina yake hata nikiwa nje nitajua matokeo.”
Shabiki kindakindaki wa Yanga na Stars anayejulikana kwa jina maarufu la Utopolo amesema: “Tiketi ninayo lakini amshaamsha ninazofanya hapa nje ni jukumu langu kama Mtanzania wakati tunasubili askari wetu wapambane.”