Kwa Mkapa usalama freshi, mashabiki mdogomdogo

LICHA ya kutokuwa na vaibu kubwa la mashabiki kwa sasa, lakini hali ya usalama kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa utakaotumika kwa pambano la ufunguzi wa michuano ya CHAN kati ya Taifa Stars na Burkina Faso ni ya aina yake kutokana na polisi kuwa kila kona kuhakikisha hakutokei kihatarishi cha usalama.

Leo, Agosti 2, 2025 Tanzania kuanzia saa 2:00 usiku, Uwanja wa Benjamin Mkapa Stars itakuwa inapeperusha bendera ya taifa.

Mwanaspoti lililowahi mapema uwanjani hapo limeshuhudia hali ya usalama ikiwa shwari kwenye kila jukwaa na milango ya kuingia ndani sambamba na vyooni ambapo kuna askari wamesimama kuhakikisha kila mtu anaingia kulingana na jukwaa alilopo kwa lengo la kuhakikisha hali ya usafi na usalama.

Kama wewe unahofia vurugu ndani ya uwanja, basi usiwaze kwani askari wapo kila mahali, huku mashabiki wakisogea mdogo mdogo kuingia ndani ya uwanja kushuhudia pambano hilo.

Polisi waliozunguka kila kona wanaonekana kujipanga vilivyo kwani wamevalia beji za CAF wakizingatia tiketi kama na kama mtu amekosea anapewa maelekezo ikiwamo eneo la kuingilia uwanjani.

Mashabiki wachache waliofanikiwa kuingia hadi sasa wanaendelea kupata burudani kutokana na nyimbo mbalimbali zinazopigwa kabla ya mchezo huo.