Ma RC watwishwa zigo migogoro ya ardhi Nyanda za Juu Kusini

Mbeya. Ili kuondoa migogoro ya wakulima na wafugaji Nyanda za Juu Kusini, Serikali imewataka wakuu wa Mikoa na idara kuweka na kusimamia vyema mipango ya matumizi bora ya ardhi kwa wananchi.

Akizungumza leo Jumamosi Agosti 2, 2025 kwa niaba ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Beno Malisa amesema ili kuondokana na migogoro ya wakulima na wafugaji, wakuu wa mikoa na idara wanapaswa kusimamia vyema mipango ya matumizi bora ya ardhi.

Amesema kanda hiyo imekuwa na uzalishaji bora wa chakula hadi kufikia ziada ya tani zaidi ya 99 milioni na amewaomba wananchi kuweka akiba kwa ajili ya familia zao.

“Tuepuke kuuza chakula chote, tunapaswa kuweka na ziada kwa ajili ya familia, lakini tuepuke kuvuna mazao yakiwa bado muda wake haswa upande wa Pareto,” amesema Malisa.

Amewasihi wakulima kuwatumia vema maafisa ugani pindi wanapohitaji kutumia  viuatilifu na kemikali kwenye mashamba yao ili kuepuka athari zinazoweza kuathiri  afya ya binadamu na mazingira.

Mapema akitoa taarifa ya maonesho hayo, Katibu Tawala wa Mkoa wa Njombe, Judica Omary amesema wakulima na wafugaji watapata fursa ya kujifunza teknolojia mbalimbali pamoja na kusikilizwa na kutatuliwa changamoto zao.

Amesema serikali inaendelea kuwawezesha wakulima kuzalisha kwa tija na kuwahimiza matumizi ya teknolojia katika kilimo na ufugaji.

“Katika Msimu wa mavuno wa 2024/2025, Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini ilizalisha zaidi ya tani 13.140 milioni za mazao ya chakula na tani 863,178 za mazao ya biashara, mahitaji ya chakula kwa mikoa hii kwa mwaka inakadiriwa kuwa tani zaidi ya 3,141 milioni,” amesema katibu tawaka huyo.

Amesema takwimu hizo zinaonesha kuwa ziada ya chakula ni jumla ya zaidi ya tani 9,998 lakini pamoja na ziada iliyopo, bado wananchi wanaendelea kushauriwa kuweka sehemu ya ziada ya mazao ya chakula kwa ajili ya usalama wa chakula kwa ngazi ya kaya.

Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Iringa, Daud Yassin amesema kutokana na maendeleo yaliyofanywa na Serikali katika utekelezaji wa ilani, wana uhakika chama chao kitashinda tena katika uchaguzi mkuu ujao.