Dar es Salaam. Wakati mawakili wa Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu wakilalamikia vitendo walivyoeleza vya ukiukwaji wa haki dhidi ya mteja wao vinavyodaiwa kufanywa na askari Magereza, jeshi hilo limekana madai hayo.
Jeshi la Magereza katika taarifa yake limesisitiza kuwa, mahabusu au mfungwa anapokuwa chini ya himaya ya jeshi hilo, ni lazima awajibike “kufuata na kutii kanuni, miongozo na maelekezo halali anayopewa na askari” ambayo wakati wote yanalenga kuimarisha usalama.
Julai 30, 2025 ilisambaa video inayomwonyesha askari magereza akimsukuma Lissu, muda mfupi baada ya shauri dhidi yake linaloendelea katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuahirishwa.
Baadaye Agosti mosi, 2025 mawakili wa Lissu wakiongozwa na Dk Lugemeleza Nshala, walizungumza na waandishi wa habari wakilaani kitendo cha askari huyo kumsukuma mteja wao mahakamani, huku akiitaka Mahakama na Jeshi la Magereza kuchukua hatua kuzuia vitendo vinavyofanywa na askari hao.
Dk Nshala alisema kitendo cha Mahakama kuruhusu askari wa Jeshi la Magereza kuingia mahakamani wakiwa wameficha nyuso zao na kutesa watu, ikiwemo kuwasukuma ni kinyume cha sheria
“Askari wa magereza wamekuwa wanakuja mahakamani wamejifunika kininja (wakiwa wamefunika nyuso zao) na kuzunguka kizimba, kana kwamba Lissu ana hatia. Tulilalamika mbele ya hakimu mara ya kwanza, walikuwa wanakaa naye hata kizimbani, baadaye wametoka sasa wanakizingira kizimba,” alisema Dk Nshala na kuongeza:
“Tunasema hii yote inatuma dalili kwamba mahakama zetu siyo huru. Sisi kama mawakili hatuwezi kukubali kuwa sehemu ya mahakama ambazo haziko huru.”
Dk Nshala alisema wamechukua hatua kwa kumwandikia Jaji Mkuu kumtaka arekebishe hali hiyo, huku wakimtaka Mkuu wa Jeshi la Magereza kuliangalia suala hilo kwa sababu kitendo hicho kimedhalilisha si tu mhimili wa Mahakama, bali pia kutoa picha halisi ya jinsi ambavyo kuna askari wanaofanya vitendo visivyostahili.
Mbali ya mawakili hao, Chama cha Mawakili wa Tanganyika (TLS) pia kilitoa tamko kuhusu tukio hilo kikieleza vitendo vinavyofanywa na vyombo vya dola chini ya ulinzi wa Jeshi la Magereza ni ukikwaji wa Katiba ibara ya 12 (2), 13(6) (b) na misingi ya Haki za Binadamu za Kimataifa.
Katika tamko hilo lililosainiwa na Rais wa TLS, Boniface Mwabukusi, wameomba kuonana na Jaji Mkuu kujadili na kusisitiza umuhimu wa kuheshimu haki, usawa na hadhi ya kila mtu.
“TLS inalitaka Jeshi la Magereza kuwajibika mara moja kwa kuzuia askari wanaoficha utambulisho wao, kuingia mahakamani na kuwachukulia hatua za kinidhamu askari wote waliohusika katika shambulio dhidi ya wakili Lissu Julai 30, 2025,” linaeleza tamko la TLS.
Jeshi la Magereza kupitia taarifa iliyotolewa leo Agosti 2, 2025 na msemaji wake, Elizabeth Mbezi imeeleza siku ya tukio hilo Lissu alikuwa akielekezwa na kuongozwa kutoka katika chumba cha mahakama tayari kwa safari ya kurudi gerezani baada ya kuonyesha dalili za kukaidi.
Taarifa hiyo imeeleza tukio hilo lilitokea baada ya hakimu anayesikiliza shauri hilo kuliahirisha na kutoka nje ya chumba cha mahakama.
“Ikumbukwe kuwa, Jeshi la Magereza ni chombo cha ulinzi na usalama chenye jukumu la msingi la kuhakikisha usalama wa mahabusu na wafungwa wote walio chini ya himaya yake, wakiwa ndani au nje ya maeneo ya magereza,” amesema na kuongeza:
“Hii inajumuisha kuwalinda dhidi ya madhara yoyote yanayoweza kutokea nje au kusababishwa na wao wenyewe. Vitendo vyote vya kiusalama vinavyochukuliwa na askari mahakamani au maeneo mengine vinalenga kutimiza wajibu huu wa kisheria.”
Kuhusu kufunika nyuso kwa mtindo wa kininja, taarifa ya Jeshi la Magereza imefafanua kuwa, umma unapaswa kufahamu kwamba jeshi hilo lina utaratibu wa kupanga matumizi ya mavazi kulingana na mazingira ya kazi au tathmini ya athari za kiusalama kwa wafungwa, mahabusu na hata askari anapotekeleza majukumu ya kazi.
Jeshi hilo limesema kwa namna yoyote mavazi hayo hayazuii mwenendo wa kesi mahakamani wala haki ya mtuhumiwa.
“Jeshi halitasita kuchukua hatua stahiki na kwa wakati katika kukabiliana na viashiria vyovyote vya changamoto za kiusalama. Usalama wa mahabusu Tundu Lissu utaendelea kuimarishwa wakati wote atakapokuwa chini ya mamlaka ya Magereza,” imeeleza taarifa hiyo