Arusha. Usemi wa Kiswahili usemao “Mganga hajigangi” umethitika baada ya mganga wa kienyeji kutoka mkoani Geita, Masoud Adam ambaye alijikuta akikosa pa kujitetea baada ya Mahakama ya Rufani kukataa rufaa aliyoiwasilisha kupinga kifungo cha miaka 30 jela alichohukumiwa kwa kosa la ubakaji.
Katika kesi ya msingi iliyosikilizwa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Geita, Masoud alishtakiwa na hatimaye kutiwa hatiani kwa kosa la kumbaka binti mwenye umri wa miaka 18, aliyekuwa amempoteza mtoto wake.
Kwa mujibu wa ushahidi uliowasilishwa mahakamani hapo, mganga huyo alimshawishi binti huyo anayefahamika kwa jina la BF katika rufaa hiyo, kuwa anaweza kumsaidia kwa kufanya matambiko ili mtoto wake arejee, kwa malipo ya Sh20,000.
BF alikubali kutoa kiasi hicho cha fedha na kuongozwa hadi nyumba ya kulala wageni, ambako mganga huyo alidai kuwa sharti lingine ni kwa binti huyo kukubli kufanye mapenzi na mwanaume ili mtoto wake apatikane.
BF pia alieleza kuwa alikataa kutekeleza ombi hilo, lakini mganga huyo alimshambulia na akampaka dawa sehemu za siri na kumbaka. Alisema alishindwa kujitetea kwa kuhofia ushirikina, hadi alipozidiwa na kupiga kelele kuomba msaada, hatimaye akaokolewa.
Rufaa dhidi ya hukumu hiyo ilisikilizwa na Mahakama ya Rufani iliyoketi jijini Mwanza kupitia rufaa namba 566 ya mwaka 2023, chini ya jopo la majaji watatu: Augustine Mwarija, Lameck Mlacha na Mustafa Ismail.
Katika uamuzi wao wa Julai 29, 2025, majaji hao walipitia hoja zote tatu za rufaa, ikiwamo ya madai ya mkanganyiko kati ya ushahidi na hati ya mashtaka.
Hata hivyo, baada ya kuchambua kwa kina ushahidi wote, walikubaliana kuwa upande wa mashtaka uliweza kuthibitisha kesi hiyo bila shaka yoyote na kwamba, hakukuwa na mkanganyiko ulioathiri mwenendo wa haki.
Hivyo basi, Mahakama ya Rufani ilitupilia mbali rufaa hiyo na kubariki adhabu ya kifungo cha miaka 30 jela dhidi ya Masoud Adam, ikisisitiza kuwa hukumu iliyotolewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Geita ilikuwa sahihi kisheria.
Katika kesi ya msingi, mlalamikaji anayejulikana kwa jina la BF, mkazi wa Kijiji cha Mwangata Wilaya ya Bukombe, Mkoa wa Geita, alimpoteza mtoto wake Desemba, 2020.
Akiwa na matumaini ya kumpata mtoto huyo, BF alimtafuta Masoud aliyejitambulisha kama mganga wa kienyeji na kudai kuwa akimlipa Sh20,000 angeweza kumrejeshea mtoto huyo kwa kufanya matambiko.
Masoud alimweleza BF kuwa matambiko hayo yalihitaji kusafiri hadi Bukombe na Desemba 15, 2020, walifika eneo hilo na kufikia katika nyumba ya kulala wageni ya Kapera, walikopokelewa na shahidi wa tatu, Neema Makelemo, mhudumu wa nyumba hiyo. BF alipewa chumba namba mbili na Masoud alimtambulisha kuwa ni mke wake.
BF alieleza mahakamani kuwa waliingia katika chumba hicho saa 10 alfajiri na akiwa ndani ya chumba, Masoud alimwambia ili masharti yaweze kutimia, lazima afanye mapenzi na mwanaume yeyote ili aweze kumuona mtoto wake aliyepotea huku akimtaka afanye naye mapenzi.
BF alikataa, ndipo Masoud akaamua kumpiga huku akimlazimisha kufanya naye mapenzi, akapaka dawa kwenye uume wake na kumbaka mara kadhaa.
BF alisema baadaye alipata nguvu, akapiga kelele na akafanikiwa kutoka nje ya chumba hicho akiomba msaada.
Alidai kuwa kelele hizo zilimfanya shahidi wa tatu kumjulisha mmiliki wa nyumba ya kulala wageni, Zakaria Bwire. Walitoka na kumkuta BF nje akiwa analia, ndipo simu ikapigwa polisi.
Shahidi wa nne, Inspekta Maulid alifika eneo la tukio na kumtaka Masoud afungue mlango wa chumba, lakini alikataa. Polisi walivunja mlango na kumkuta akiwa na vifaa mbalimbali vya uganga.
Masoud alieleza kuwa yeye ni mganga wa kienyeji, lakini alishindwa kuwasilisha leseni yoyote ya kuthibitisha kazi hiyo. Alikamatwa na kuwekwa chini ya ulinzi huku BF akipelekwa hospitalini kwa ajili ya uchunguzi wa kitabibu.
Kwa kuzingatia ushahidi huo, Mahakama ya Rufani ilithibitisha kuwa hukumu ya awali ilizingatia misingi ya haki na sheria na hivyo kutupilia mbali rufaa hiyo ya pili ya Masoud, ikisisitiza kuwa ushahidi dhidi yake ulikuwa wa kutosha.
Katika utetezi wake mbele ya Mahakama, Masoud Adam alikiri kuwa aliwahi kufika katika nyumba ya kulala wageni ya Kapera, lakini alikana kutenda kosa la ubakaji aliloshitakiwa nalo.
Alidai kuwa siku ya tukio alichukua chumba katika nyumba hiyo, kisha alitoka kwenda kutafuta chakula. Kwa mujibu wa maelezo yake, wakati akiwa amerudi chumbani, polisi walivamia na kufanya upekuzi wa chumba hicho.
Masoud alieleza kuwa baada ya hapo alikamatwa na kupelekwa kituo cha polisi ambako alikaa kwa siku tatu.
Alidai kuwa akiwa kituoni alipewa karatasi ya kusaini lakini hakuelezwa wala kuelewa kilichoandikwa ndani yake. Pia alikana kumfahamu mlalamikaji (BF), akidai kwamba alimwona kwa mara ya kwanza akiwa mahakamani.
Hata hivyo, Mahakama ya Wilaya pamoja na Mahakama ya Hakimu Mkazi aliyeteuliwa kwa mamlaka maalum ya kusikiliza kesi hiyo, zilipitia ushahidi wa pande zote na hatimaye kumtia hatiani Masoud. Mahakama hizo zilieleza kuwa ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka ulikuwa thabiti na ulitosha kumtia hatiani kwa kosa la ubakaji.
Katika rufaa yake iliyosikilizwa na Mahakama ya Rufani, Masoud Adam aliwasilisha sababu tatu kuu za kupinga hukumu ya awali iliyomtia hatiani kwa kosa la ubakaji.
Sababu ya kwanza ilidai kuwa ushahidi wa mashahidi katika rekodi ya kesi ulirekodiwa kinyume na matakwa ya Kifungu cha 210 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA). Sababu ya pili, kulikuwa na tofauti kati ya hati ya mashtaka na ushahidi uliotolewa mahakamani, ikielezwa kuwa kulikuwa na herufi moja iliyoachwa katika jina la mlalamikaji.
Sababu ya tatu ilihusiana na madai kwamba maelezo ya onyo ya mrufani yalichukuliwa bila kuzingatia matakwa ya Kifungu cha 58(1)(a) na 50(1) vya CPA.
Katika rufaa hiyo, Masoud alijiwakilisha mwenyewe bila msaada wa wakili, huku upande wa Serikali ukiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi Luciana Shaban, akiwa na wakili mwenzake.
Jopo la majaji likiongozwa na Jaji Lameck Mlacha baada ya kupitia kumbukumbu za kesi na sababu za rufaa, alisema kwa mujibu wa Kifungu cha 210 CPA, kinatoa mwongozo kuhusu jinsi ushahidi wa mashahidi unavyopaswa kurekodiwa mbele ya mahakama.
“Baada ya uchambuzi wa rekodi, ilibainika kuwa utaratibu huo ulifuatwa kikamilifu na hivyo hoja hiyo naitupilia mbali,” alisema.
Akijibu hoja ya tofauti kati ya shtaka na ushahidi, Jaji Mlacha alibainisha kuwa tofauti hiyo ilikuwa ni ya herufi moja katika jina la mlalamikaji jambo ambalo halikuathiri uelewa wa kesi wala kusababisha mkanganyiko wa kisheria. Hivyo, alisema kosa hilo halikuwa na uzito wa kuathiri mchakato wa haki.
Kuhusu hoja kuwa maelezo hayo yalichukuliwa bila kuzingatia masharti ya CPA, Jaji Mlacha alisema rekodi zinaonyesha Masoud hakuwa na uelewa wa kusoma na kuandika na kwamba, maelezo hayo yalisomwa kwake kabla ya kusaini kwa alama ya kidole gumba.
“Kwa mujibu wa kifungu cha 58(4) cha CPA, polisi walikuwa na mamlaka ya kurekodi maelezo hayo kwa njia hiyo. Mahakama ilikubaliana na hoja ya upande wa mashtaka kuwa sheria hiyo ilifuatwa ipasavyo,” alisema jaji huyo.
Aliongeza kuwa kuhusu Kifungu cha 50(1) cha CPA, ingawa hakukuwa na ushahidi wa moja kwa moja unaoonyesha muda halisi wa kukamatwa na kufikishwa kituo cha polisi, mazingira ya tukio yanaonyesha kuwa polisi walifika eneo la tukio haraka, na ndani ya dakika 40 walikuwa tayari wameanza kurekodi maelezo ya onyo, hivyo hakuna ushahidi wa ukiukwaji wa masharti hayo.
Kwa kuzingatia hoja hizo zote, Mahakama ya Rufani ilihitimisha kuwa rufaa ya Masoud Adam haina msingi wa kisheria na ikaamuru itupiliwe mbali, hivyo kuthibitisha tena adhabu ya kifungo cha miaka 30 jela dhidi yake.