Ikiwa leo ndiyo siku ya kuanza kwa mashindano ya CHAN 2024, macho ya wengi Afrika na dunia yataelekezwa Tanzania, ambayo kwa mara ya kwanza inakuwa mwenyeji wa fainali hizi pamoja na Kenya na Uganda, ikiwa na kocha mzawa kwa mara ya kwanza kwenye michuano hiyo.
Kwa Kocha Mkuu Hemed Suleiman maarufu kama ‘Morocco’, mashindano haya hayawakilishi tu heshima ya kuwa wenyeji, bali ni mwanzo mpya wa safari ya kisoka la Tanzania na heshima kwa kila mmoja aliyepambana kuhakikisha yanafanyika.
Mwanaspoti limefanya mahojiano maalumu na Morocco aliyewahi pia kuzifundisha klabu mbalimbali kubwa nchini, akisema matarajio yake ni kuona timu hiyo inafanya vizuri kuanzia mchezo wa kwanza hadi wa mwisho wa mashindano hayo.
“Kuwa mwenyeji pamoja na Kenya na Uganda ni heshima kubwa kwa Tanzania. Lakini zaidi ya yote, ni nafasi ya kuonyesha juhudi zinazofanywa na klabu zetu kama Simba, Yanga, Azam na nyingine katika kukuza vipaji vya ndani. Mashindano haya yamechochea maendeleo kwenye miundombinu, mafunzo na hata uwekezaji,” anasema Morocco ambaye ameshaiongoza Stars kushinda michezo minne ya kujiandaa na michuano hii.
Hata hivyo, imekuwa ikielezwa Taifa Stars ipo kundi gumu na ni nadra kufuzu hatua inayofuata, Tanzania ipo na Burkina Faso, Mauritania, Jamhuri ya Afrika ya Kati na Madagascar timu ambazo zinaonekana zina uwezo wa juu.
“Kwenye soka la kisasa hakuna mpinzani mrahisi wala mgumu. Timu zote zimejaa vipaji na mbinu nzuri za kiufundi. Tumeziangalia kwa makini, tunajua wanakuja na nguvu na kasi. Tutazipa kila moja heshima inayostahili lakini hatutakuwa na huruma uwanjani, tumejiandaa kwenye kila eneo kuhakikisha tunawapa heshima mashabiki wetu watakaojazana Uwanja wa Mkapa kutuunga mkono.”
Morocco anasema pamoja na kwamba kila timu imejiandaa vizuri, lakini kwao CHAN si jukwaa la kusaka matokeo pekee bali pia ni darasa la kutengeneza msingi wa kikosi imara cha Taifa Stars kwa miaka ijayo, kwa kuwa baada ya muda mfupi Tanzania itaandaa michuano ya Kombe la Mataifa Afrika AFCON 2027.
“Tuna wachezaji kutoka klabu ambazo zimezoea mashindano ya CAF, tuna wachezaji kutoka Simba, Yanga, Azam na nyingine nyingi ambazo zina uzoefu wa kutosha. CHAN inawapa fursa ya kujipima kwa ngazi ya kimataifa na kujiimarisha kwa ajili ya AFCON 2027. Tunaangalia namna wanavyocheza, nidhamu yao, uongozi wao, haya yote ni sehemu ya mchakato wa muda mrefu, tunakwenda kutafuta ushindi, lakini tukifahamu kuwa mbele tuna kazi kubwa zaidi ya kufanya,” alisema kocha huyo ambaye aliiwezesha Stars kucheza AFCON 2025 Morocco na kutolewa hatua ya makundi.
Akizungumzia kuhusu kikosi chake Morocco anasema licha ya msimu mrefu wa Ligi Kuu, wachezaji wako katika hali nzuri kimwili na kiakili kutokana na maandalizi ya kina, ikiwemo kambi maalumu waliyoweka Misri pamoja na Arusha.
“Ligi yetu ni ngumu na imewaandaa vizuri. Pia tumeweka mifumo ya kusaidia wachezaji kisaikolojia ili wawe tayari kwa presha ya mashindano makubwa. Kikosi hiki kimejengwa kwa misingi ya maadili, nidhamu na kupigana kwa ajili ya Taifa.
“Safu yetu ya ulinzi imejaa wazoefu. Tuna viungo wenye nguvu na mbinu za kusukuma mpira kwa ufasaha. Kwenye ushambuliaji bado tunatengeneza muunganiko, lakini dalili ni njema. Kilicho bora zaidi ni uongozi katika kikosi. Tuna vijana wenye ukomavu na weledi mkubwa ambao tunaamini wanaweza kulipa heshima taifa lao.”
Tanzania imeshiriki CHAN mara mbili kabla ya mwaka huu (2009, 2020) lakini haijawahi kufuzu hatua ya mtoano. Morocco anaamini mara hii ni tofauti kwani maandalizi yao ni mazuri zaidi na wana kila sababu ya kuweka rekodi kwa kuwa wao ndiyo waandaaji na kila mmoja anawatazama watafanya nini.
“Tuna sapoti ya nyumbani, maandalizi mazuri na kikosi bora zaidi. Hii ni nafasi yetu ya kuandika historia mpya. Hatuchukulii chochote kimzaha. Tunataka kwenda mbali na kuandika ukurasa mpya kwenye historia ya soka la Tanzania, lakini ni ‘room’ maalum kwa wachezaji wetu kujitangaza na kujiuza nje, lazima nao tuwatengenezee uwanja mpana wa kupata mafanikio yao binafsi.”