NIRC yaja na Teknolojia Mpya za Umwagiliji Nane Nane Dodoma, 2025

…………….

📍NIRC:Dodoma

Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC)imewasilisha teknolojia mpya za kisasa za umwagiliaji katika kijiji cha Mitambo kwenye maonyesho ya nanenane Dodoma.

Teknolojia hizo ni pamoja na mitambo ya umwagiliaji kwa njia ya mvua (CENTER PIVOT), mashine za uchimbaji wa visima, mabwawa na umwagiliaji kwa njia mbalimbali ikiwemo za matone, lengo ni kutoa elimu ya umwagiliaji katika Maonesho ya Kilimo ya Nanenane mwaka huu, ikiwa ni sehemu ya juhudi za mageuzi ya sekta ya kilimo kupitia matumizi ya teknolojia bunifu. 

Akizungumza katika viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Tume hiyo ambaye pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimali, Maria Itembe, amesema teknolojia hiyo ni mpya kwa matumizi ya taasisi hiyo, ambapo imekuwa ikitumika kwa mataifa mbalimbali lengo likiwa ni kuleta mageuzi katika kilimo cha Umwagiliaji

Amesema  Tume inashiriki katika maonesho kitaifa Nane nane, katika viwanja vya Nzuguni, hapa Dodoma na inatoa wito kwa wakulima na wadau wote wa kilimo kutembelea mambanda ya NIRC ili kujifunza na kuhamasisha matumizi ya rasililimali ya maji kupitia teknolojia za kisasa za umwagiliaji.

Itembe ameongeza kuwa Tume inatambua umuhimu wa kuendeleza sekta ya kilimo kupitia umwagiliaji, kama sehemu ya mkakati wa kuhakikisha usalama wa chakula, kuongeza kipato cha wananchi na kukuza mchango wa kilimo katika pato la Taifa na tumepokea maelekezo ya Makamu wa Rais, Dkt. Philip Mpango, kwa taasisi za umma kuimarisha elimu, utafiti na teknolojia zinazoleta tija kwa wakulima, na kwetu katika maonyesho ya Nane Nane 2025 ni fursa mahsusi ya kuwafikia wananchi kwa elimu ya vitendo na teknolojia bunifu. 

Amesema kuwa Tume imejipanga kutoa elimu ya kitaalamu na kuhamasisha matumizi ya teknolojia bunifu za umwagiliaji ili wakulima waweze kuongeza uzalishaji, kipato na ustawi wa kiuchumi na taifa kwa ujumla.

 “Mwaka huu tumekuja na vitu vingi vipya tunacho kijiji cha mitambo ambapo kuna mitambo mbalimbali ikiwemo mfumo wa umwagiliaji wa mvua, magari yenye mitambo za uchimbaji visima, mabwawa na mengine mengi ambayo hayakuwepo maonyesho yaliyopita. Nyuma yangu kuna mitambo mikubwa ya kumwagilia – hii ni Center Pivot, teknolojia mpya tunayoweka kwa sasa katika maeneo ya umwagiliaji,” amesema Itembe.

 Ameongeza kuwa teknolojia hiyo tayari imeanza kufungwa katika mashamba mbalimbali ya miradi ya umwagiliaji  ikiwa ni utekelezaji wa agizo la serikali kuhusu matumizi ya teknolojia za kisasa katika sekta ya kilimo, kama sehemu ya kuongeza tija na uzalishaji. 

“Tume tunaamini kupitia mitambo iliyopo, wakulima wataweza kujifunza mengi na kufikiwa na huduma za Umwagiliaji katika maeneo yao, kwani fursa hizi zipo kila mahali mikoani kote tumewafikia hivyo ni wakati sasa Watanzania kuchangamkia fursa za Kilimo cha Umwagiliaji kwa kulima mwaka mzima bila kutegemea mvua,” 

Amesisitiza kuwa licha ya gharama kubwa za ununuzi wa mitambo ya kisasa, hatua hiyo imewezekana kutokana na uamuzi wa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kuongeza bajeti na kuwekeza kwa dhati katika sekta ya umwagiliaji.

 Kwa mujibu wa Itembe, matumizi ya teknolojia hiyo yataongeza ufanisi wa kilimo kwa kulima zaidi ya mara moja kwa mwaka hivyo kuongeza utoshelevu wa chakula na kuchochea  ukuaji wa uchumi.

Pia, Tume inashirikiana na sekta binafsi kusambaza teknolojia mpya za umwagiliaji, zitakazo tumia maji kwa ufanisi na kuleta tija kwenye kilimo, kufuatilia utekelezaji wa sera za kilimo biashara na kuendeleza matumizi bora ya maji na mbinu za kukabili mabadiliko ya tabianchi, kwa lengo la kuifanya Tanzania iwe kitovu cha uzalishaji wa chakula barani Afrika na duniani kote. 

Amesisitiza kuwa licha ya gharama kubwa za ununuzi wa mitambo ya kisasa, hatua hiyo imewezekana kutokana na uamuzi wa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kuongeza bajeti na kuwekeza kwa dhati katika sekta ya umwagiliaji