Dar es Salaam. Mahakama Kuu Masjala Ndogo Musoma imemuondolea hatia mfungwa Paulo Azimio Kisike, aliyekuwa amehukumiwa kifungo cha miaka saba jela kwa kosa la utekaji.
Hukumu hiyo imetolewa na Jaji Marlin Komba baada ya kukubaliana na rufaa aliyoikata kupinga hatia hiyo, kuwa Jamhuri haikuweza kuthibitisha shtaka hilo, rufaa ambayo iliungwa mkono na Jamhuri yenyewe iliyomshtaki.
Paulo, mkazi wa Muhimu, wilayani Serengeti, Mkoa wa Mara alihukumiwa adhabu hiyo na Mahakama ya Wilaya ya Serengeti, kufuatia kesi ya jinai namba 35714 ya 2024.
Katika kesi hiyo, Paulo alishtakiwa kwa kosa la utekaji nyara kinyume na Kifungu cha 133 cha Kanuni ya Adhabu [Sura 16, Marejeo ya mwaka 2022 sasa 2023].
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka pamoja na ushahidi wa upande wa mashtaka, wakati wa usikilizwaji kesi hiyo, mshtakiwa alitenda kosa hilo Desemba 12, 2024 katika mji wa Mugumu ndani ya Wilaya ya Serengeti mkoani Mara.
Siku hiyo mshtakiwa alimchukua kwa nguvu na kumzuia, msichana mwenye umri wa miaka 15 katika nyumba ya wageni ya Meya iliyoko mji wa Mugumu kwa nia ya kufanya naye ngono bila ridhaa yake.
Kesho yake Desemba 13, 2024 saa 2:00 asubuhi, mshtakiwa alimrudisha nyumbani kwa wazazi wake, lakini akakamatwa na mama wa binti hiyo kisha akapelekwa katika kituo cha polisi.
Kisha alipandishwa kizimbani ambako katika Mahakama ya Wilaya ya Serengeti na kusomewa shtaka kwa kosa la utekaji nyara, ambalo alilikana.
Wakati wa usikilizwaji wa kesi hiyo, upande wa mashtaka katika kuthibitisha shtaka hilo, uliwaita mashahidi watatu na upande wa utetezi ulikuwa na mashahidi wawili.
Mahakama baada ya kukamilisha usikilizaji iliridhika upande wa mashtaka uweza kuthibitisha kesi yao pasipo shaka, na ushahidi wa utetezi haukuweza kuzua shaka yoyote juu ya shtaka lililomkabili mshtakiwa.
Hivyo ilimtia hatiani na kumhukumu adhabu ya kifungo cha miaka saba jela.
Hata hivyo, Paulo hakuridhika na hukumu hiyo, hivyo alikata rufaa Mahakama Kuu, kupinga hatia huku akitoa sababu mbili za rufaa.
Katika sababu hizo alidai, hakimu wa Mahakama ya chini (Wilaya) alikosea kisheria na kimantiki kumtia hatiani na kumhukumu adhabu hiyo kwa sababu:
Mosi, kwamba upande wa mashtaka haukuweza kuthibitisha kesi dhidi yake pasipo shaka ya msingi na mbili, kwamba hakumpa fursa ya kuita shahidi wakati wa utetezi wake.
Wakati usikilizwaji wa rufaa hiyo, mrufani hakuwa na uwakilishi wa wakili na upande wa Jamhuri uliwakilishwa, Wakili wa Serikali Mwandamizi Grace Madikenya.
Mrufani alipopewa nafasi, alisema kwa kifupi kuwa hakutenda kosa la utekaji nyara na akaomba mahakama iaamuru aachiliwe huru.
Jamhuri (Serikali) kupitia Wakili Grace iliunga mkono rufaa hiyo, hususan sababu ya kwanza ya rufaa.
Wakili Grace alikubaliana na mrufani kuwa Jamhuri ilishindwa kuthibitisha kosa dhidi ya dhidi yake pasipo shaka ya msingi.
Alifafanua mrufani alishtakiwa chini ya kifungu cha 133 cha Kanuni ya Adhabu, na kwamba ili kuthibitisha kosa hilo, upande wa mashtaka ulipaswa kuthibitisha viini vitatu vya kosa hilo.
Alivibainisha kuwa Mosi, mshtakiwa alimteka mlalamikaji muathirika yaani binti huyo; mbili, utekaji huo ulikuwa kwa nia ya kufunga ndoa au kufanya naye ngono, na tatu, matumizi ya nguvu katika kutekeleza utekaji huo.
Wakili Grace alieleza katika ushahidi wa muathirika ambaye alikuwa shahidi mkuu, hakuna ushahidi wowote unaothibisha vipengele hivyo vilivyotajwa hapo juu.
Alieleza kuwa badala yake ushahidi unaonyesha kuwa muathirika alikwenda na mshtakiwa kwa hiari, na hakusema kuwa alizuiliwa na mshtakiwa wala kuwa alilazimishwa kufanya naye ngono.
Hivyo alihitimisha anaunga mkono kikamilifu rufaa hiyo katika sababu hiyo ya kwanza na kwamba rufaa hiyo mashiko.
Jaji Komba katika hukumu yake aliyoitoa Julai 28, 2025 amekubaliana na sababu ya kwanza ya rufaa hiyo na kwamba katika hukumu hiyo atazingatia sababu hiyo pekee kwani anaona kuwa ina mashiko kama ilivyoelezwa na Wakili Grace.
Jaji Komba amenukuu kifungu cha 133 cha Kanuni ya Adhabu, amba kinasema kiwa:
“Mtu yeyote ambaye kwa nia ya kufunga ndoa au kufanya tendo la ndoa na mwanamke wa umri wowote, au kumsababisha aolewe au afanye tendo la ndoa na mtu mwingine, anapomchukua kwa nguvu au kumzuia kinyume na ridhaa yake, anakuwa ametenda kosa na anastahili kifungo cha miaka saba jela.”
Amesema kuwa hiyo ili kuthibitisha kosa hilo, upande wa mashtaka una jukumu la kuthibitisha viini vitatu vilivyoainishwa katika kifungu hicho.
Pia, Jaji Komba huku akirejea kesi mbalimbali, amesema kuwa kwa kuwa mahakama hiyo ni mahakama ya kwanza ya rufaa, ina mamlaka ya kusoma na kuchambua upya ushahidi wote kabla ya kutoa uamuzi.
Amesema kuwa kwa kuangalia ushahidi wa shahidi wa kwanza wa upande wa mashtaka (PW1), yaani mwathirika, na ushahidi wote, hakuna viini hivyo vyote vitatu vya kosa hilo iwe ni kupitia ushahidi wa PW1 au mashahidi wengine.
“Ushahidi hauonyeshi kuwa muathirika alichukuliwa na kuzuiliwa kinyume na matakwa yake, au kuwa lengo lilikuwa kufunga naye ndoa au kufanya naye ngono. Mwasiriwa alikwenda mwenyewe katika nyumba ya wageni pamoja na mrufani na walilala huko; hakuna ushahidi zaidi unaopendekeza vinginevyo”, amesema Jaji Komba.
Amesema kuwa kama Sheria inavyoelekeza pamoja na kesi mbalimbali za rejea, ambazo amezitaja baadhi yake, katika kesi ya jinai, dhima ya kuthibitisha kosa iko kwa upande wa mashtaka kuthibitisha kesi dhidi ya mshtakiwa pasipo shaka ya msingi.
Jaji Komba amesema kwa kuzingatia yote yaliyoelezwa, rufaa hiyo ina mashiko.
Amesema kuwa mahakama ya awali ilikosea kwa kumtia hatiani mrufani bila kujiridhisha kuwa viini vya kosa chini ya kifungu cha 133 cha Kanuni ya Adhabu vilithibitishwa pasipo shaka ya msingi.
“Kwa kuzingatia ushahidi ulio kwenye kumbukumbu, ninakubali rufaa hii, ninatengua hukumu ya hatia na naondoa adhabu iliyotolewa,” amesema Jaji Komba na kuamuru:
“Ninamuru mrufani aachiliwe huru mara moja kutoka gerezani isipokuwa kama anashikiliwa kwa sababu nyingine halali kisheria.”