WAKATI ikibakia saa chache kabla ya kushuhudia mechi ya ufunguzi wa michuano ya Fainali za Ubingwa kwa Mataifa ya Afrika (CHAN) 2024 kati ya wenyeji timu ya taifa ya Tanzania maarufu Taifa Stars dhidi ya Burkina Faso, kikosi cha Stars kinaingia kusaka rekodi mpya kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.
Rekodi ambayo Taifa Stars inaisaka leo ni ya kushinda mechi ya ufunguzi, kwani mara mbili ilizoshiriki haijawahi kufanya hivyo, jambo linalosubiriwa kuona wakati itakapoikabili Burkina Faso kuanzia saa 2:00 usiku huu.
Fainali za mwaka huu zinakuwa ni za tatu kwa Tanzania kushiriki baada ya kufanya hivyo mwaka 2009 ilipoishia hatua ya makundi, ikimaliza nafasi ya tatu na pointi nne.
Katika fainali za mwaka 2009, Stars ilipangwa kundi A sambamba na timu za Zambia, Senegal na wenyeji wa michuano hiyo, Ivory Coast.
Mechi ya kwanza kwa Stars, iliyopigwa Februari 22, 2009, ilifungua michuano vibaya baada ya kuchapwa bao 1-0 dhidi ya Senegal.
Fainali za mwaka huo wa 2009, zilishuhudia DR Congo ikitwaa taji la kwanza la michuano hiyo, baada ya kuifunga Ghana mabao 2-0.
Baada ya hapo, Tanzania ikashiriki tena mwaka 2020 na kuishia hatua ya makundi, ilipomaliza nafasi ya tatu kundi D na pointi nne, nyuma ya Guinea iliyoongoza na pointi tano sawa na Zambia iliyomaliza ya pili, huku Namibia ikiburuza mkia na pointi moja.
Katika mechi ya kwanza iliyopigwa Januari 19, 2021, Stars ikaanza tena kwa kichapo baada ya kufungwa mabao 2-0 dhidi ya Zambia na kuendeleza rekodi mbovu mara zote mbili iliposhiriki michuano hiyo.
Fainali hizo za 2020 zilifanyika Cameroon, ambapo mabingwa walikuwa Morocco iliyoichapa Mali mabao 2-0 na kutetea taji hilo baada ya kulichukua mwaka 2018.
Katika Chan 2024, Tanzania ipo Kundi B pamoja na Madagascar, Mauritania, Burkina Faso na Jamhuri ya Afrika ya Kati. Tanzania ni mwenyeji wa michuano hiyo kwa kushirikiana na Kenya na Uganda.