TIMU ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars, imeanza vyema Fainali za Ubingwa wa Afrika kwa Wachezaji wa Ndani CHAN, baada ya kuichapa Burkina Faso mabao 2-0.
Mabao mawili ya kila kipindi yametosha kuipa Stars ushindi huo muhimu, ikitawala vizuri mchezo huo ukipigwa leo Agosti 2, 2025 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar.
Stars bao lake la kwanza limefungwa dakika ya 45+2 na mshambuliaji Abdul Suleiman ‘Sopu’ kwa mkwaju wa penalti iliyotokana na beki wa Burkina Faso, Franc Tologo kumchezea vibaya mshambuliaji wa Stars, Clement Mzize.
Bao hilo limekuwa la kwanza kwenye fainali hizi za msimu wa nane, zinazoandaliwa kwa umoja wa mataifa matatu ya Tanzania, Kenya na Uganda Kenya.
Mpaka mapumziko, Stars iliyotawala kipindi hicho ilitoka na uongozi wa bao 1-0 huku ikipoteza nafasi nyingi za kufunga.
Kipindi cha pili Stars ikarudi na mpango uleule wa kutafuta mabao zaidi, ikiendelea kutengeneza nafasi nyingi za kufunga lakini ikashindwa kutulia na kuzitumia.
Wenyeji wakapata bao la pili dakika ya 71 mfungaji akiwa beki Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ akimalizia kwa kichwa krosi ya Idd Seleiman ‘Nado’
Kabla ya kuruhusiwa kwa bao hilo, Stars ililazimika kusubiri kwa dakika moja kukubaliwa kufuatia kutakiwa kuthibitishwa na VAR na hatimaye likapita na kuibua shangwe.
Bao hilo Stars limeonyesha hesabu sahihi za kujenga mashambulizi ambapo mabao yote mawili yametengenezwa upande wa winga ya kushoto kupika ushindi huo.
Mchezo huo wa ufunguzi kundi B, umehudhuriwa na maelfu ya mashabiki lakini wakashindwa kuujaza uwanja huo huku mgeni rasmi akiwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, aliyeambatana na Rais mstaafu Dk Jakaya Kikwete.
Rais wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF), Dk Patrice Motsepe naye alikuwa sehemu ya waliohudhuria ufunguzi huo akiambatana na mwenyeji wake Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia.