TANESCO Ruvuma Yatoa Elimu kwa Wananchi Kuhusu Matumizi sahihi ya Umeme na Nishati Safi ya kupikia.

Mbinga, Ruvuma 

Shirika la Umeme Tanzania TANESCO Mkoa wa Ruvuma limetoa elimu kwa wananchi wa Kijiji cha Linda kuhusu matumizi salama ya umeme, ulinzi wa miundombinu ya umeme na umuhimu wa kutumia nishati safi ya kupikia.

Zoezi hilo la utoaji elimu limefanyika katika Kata ya Linda, Wilaya ya Mbinga, likihusisha maafisa huduma kwa wateja wasaidizi kutoka ofisi ya Afisa Uhusiano na Huduma kwa Wateja TANESCO Mkoa wa Ruvuma, ambao ni Emma Ulendo, Getruda Mrango na Bertha Sahi.

Akizungumza Emma Ulendo, mmoja wa maafisa waliotoa elimu hiyo, amesema matumizi ya nishati safi ya kupikia ni muhimu si tu kwa afya za wananchi, bali pia kwa kulinda mazingira.

“Tunawahimiza wananchi kupunguza matumizi ya kuni na mkaa na badala yake watumie umeme kwa kupikia, ili kupunguza uharibifu wa misitu na pia kujikinga na magonjwa ya mfumo wa upumuaji yanayosababishwa na moshi wa kuni, kupikia umeme ni rahisi na nafuu zaidi kuliko nishati zingine ,” 

Kwa upande wake, Getruda Mrango amesisitiza umuhimu wa kuzingatia usalama wa umeme majumbani na kutoa wito kwa wananchi kuhakikisha wanaepuka matumizi hatarishi,

“Ni muhimu kutumia vifaa vya umeme kwa usahihi, ni hatari  kuunganisha umeme kiholela vinaweza kusababisha ajali kubwa,” 

Naye Bertha Sahi ameeleza hatua zinazopaswa kufuatwa na mteja mpya anayetaka kuunganishiwa umeme, akibainisha kuwa kuna mfumo rasmi na rahisi wa kuwasilisha maombi.

“Tumeeleza jinsi ya kujaza fomu za maombi, pamoja na muda wa kusubiri kufikishiwa  huduma. Tunataka kila mwananchi ajue hatua hizi ili kuepusha matapeli na vishoka,” alisema Sahi.

Maafisa hao pia wamehimiza ulinzi wa miundombinu ya umeme na kuwahamasisha wananchi kutoa taarifa wanapobaini vitendo vya wizi au uharibifu wa nguzo, nyaya au transfoma.

Wananchi wa Kijiji cha Linda wameipongeza TANESCO kwa kufika kijijini hapo na kutoa elimu hiyo muhimu. Wamesema kuwa mafunzo hayo yameongeza uelewa wao kuhusu matumizi salama ya umeme na wameomba elimu hiyo ifikishwe pia kwenye vijiji vingine vya Mkoa wa Ruvuma.