MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA)imezitaka taasisi za Umma kulipa kodi stahiki na kwa wakati kwani kuwa taasisi ya serikali hakutoi uhalali wa kuwa juu ya sheria.
Vilevile, mamlaka hiyo imeweka bayana kuwa inaweza kusamehe kipato kisitozwe kodi ili kuwezesha ukuaji wa biashara, lakini haiwezi kusamehe wala kufuta kodi iliyokwisha kuwepo kwa mujibu wa sheria.
Kauli hiyo imetolewa juzi na Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Mwenda, alipokuwa akizungumza na wafanyabiashara, watumishi wa taasisi za umma, pamoja na mameneja wa TRA kutoka mikoa mbalimbali,Mkutano uliofanyika Dar es salaam.
“Kuwa taasisi ya serikali hakukupi haki ya kuwa juu ya sheria. Kama unafanya shughuli ya kiuchumi ambayo haijasamehewa na inafanana na ile ya sekta binafsi, basi una wajibu wa kulipa kodi kama wengine. Mfumo wa kodi unapaswa kuwa wa usawa kwa wote,” alisema Mwenda.
Aliongeza,”Ninyi ni mashahidi wengi wenu wanalalamika hatujalipwa mishahara sijui nini sasa mtalipwaje kama hamjakusanya mapato ?kusanyeni kwa umakini ilituweze kuondoa malalamiko hayo,”alisema Mwenda
Alisisitiza kuwa kufuta kodi si jambo linalowezekana kwa mujibu wa sheria, na hata Waziri wa Fedha hana mamlaka ya kufanya hivyo.
“Suala la kodi ni la kisheria. Waziri anaweza kusamehe kipato kisitozwe kodi kabla ya kodi kuanza kutozwa, lakini hawezi kusamehe kodi ambayo tayari inadaiwa. Hiyo ni fedha ya Watanzania lakini kinachoumiza zaidi ninyi ni familia mnafanya kazi kwa pamoja inatokea mmoja kati yenu anakuja kuomba kusamehewa penati tukawasamehe wote mmoja anamaliza madeni yake ya nyuma lakini mwingi akabaki na deni baadae anakuja kuomba afutiwe tena na deni hilo basi kwa hilo niseme wazi haiwezekani kwanini mmoja alipe alafu wewe usilipe kumbuka deni alifutwi,” alisema.
Ameongeza kuwa njia bora ya kudhibiti madeni makubwa ya kodi ni kwa taasisi na walipa kodi kuhakikisha wanalipa kwa wakati.
“Hata kama mimi Kamishna ningeona ni kwa maslahi ya taifa kufuta deni la kodi, siwezi. Njia sahihi ni kuzuia lisiende mbali. Tunaweza kusamehe kipato kisitozwe kodi kwa sababu tunajua kitasaidia biashara kukua na hatimaye serikali kukusanya kodi nyingi zaidi niwasii tu wambieni Washaurini wakurugenzi wenu walipe kodi kwa wakati kwani tunachokusanya kinakuja kwenu kwani kinalipa mishahara na mambo mengine hivyo kuweni sawa na sisi kwani mnavyotusaidia ndiyo kinavyokuja kwenu pia,” alifafanua Mwenda.
Aidha, Mwenda ametoa wito kwa watendaji wakuu wa taasisi za umma kuhakikisha wanashirikiana na TRA pale wanapoanzisha shughuli mpya za kiuchumi, ili wajue namna ya kuziangalia kwa mujibu wa sheria za kodi.
TRA pia imeeleza kuwa kuna baadhi ya taasisi ambazo bado zinafanya kazi kwa mazoea, jambo ambalo linaweza kusababisha migogoro ya kikodi. Hivyo, semina mbalimbali zimekuwa zikitolewa na mamlaka hiyo kwa lengo la kutoa elimu na kuondoa sintofahamu.
Akizungumzia Sheria ya Fedha (Financial Act), Kamishna Mwenda alisema kuwa sheria hiyo ya mwaka 2025 imeleta maboresho makubwa kwenye usimamizi wa kodi, hasa kwenye Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT).
“Sheria mpya imetoa wajibu mkubwa kwa Wizara ya Fedha na taasisi nyingine za serikali katika kusimamia sheria za kodi. Watumishi waliokabidhiwa jukumu la kukusanya kodi kwa niaba ya TRA wanapaswa kulitekeleza kwa uadilifu. Kutozingatia wajibu huo ni kosa la kisheria,” aliongeza.
Kwa ujumla, ujumbe wa TRA kwa taasisi za umma ni wazi usalama wa kifedha wa nchi unategemea usawa na uwajibikaji wa kila mdau wa kiuchumi, bila kujali kama ni wa serikali au binafsi.