UBUNIFU WA KISAYANSI SUA WAMVUTIA MHE. PINDA NANENANE 2025

Farida Mangube, Morogoro 

Waziri Mkuu Mstaafu, Mhe. Mizengo Pinda, ametembelea banda la Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) katika Maonesho ya Nanenane yanayofanyika kwenye Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere, mkoani Morogoro, na kuvutiwa na ubunifu na teknolojia mbalimbali zinazolenga kuboresha kilimo na maisha ya wakulima.

Katika ziara hiyo, Mhe. Pinda alipokelewa na Makamu Mkuu wa Chuo, Prof. Raphael Chibunda, ambaye alieleza kuwa SUA imeandaa jumla ya mabanda 48 yenye teknolojia na elimu tofauti zinazolenga kumsaidia mkulima kutumia mbinu za kisasa kwenye kilimo, ufugaji, lishe na afya ya wanyama.

Miongoni mwa maeneo aliyotembelea ni banda la malisho ya mifugo, ambapo alielezwa kuhusu shamba la mfano la malisho lililopo chuoni. Pia aliona maabara inayotembea, ambayo hutumika kuchukua, kuchakata na kutoa majibu ya sampuli papo kwa papo hasa kwa ajili ya kukabiliana na magonjwa ya mlipuko.

Maeneo mengine aliyotembelea ni Idara ya Lishe, ambako alipata taarifa kuhusu hali ya utapiamlo nchini na juhudi za SUA katika kushirikiana na jamii kutatua changamoto hiyo. Pia alitembelea Hospitali ya Taifa ya Wanyama na Shule ya Elimu ya Mafunzo ya Amali, ambapo alikutana na wanafunzi wa Shule ya Sekondari Mafiga wanaosomea mkondo wa Amali.

Baada ya ziara hiyo, Mhe. Pinda alisema ameridhishwa na kazi kubwa inayofanywa na SUA, hasa kwa kutumia elimu na teknolojia kutatua changamoto halisi za wakulima na wafugaji.

“Nimeridhika sana na kile nilichokiona leo. SUA inaendelea kuwa kioo cha maendeleo ya kilimo nchini. Teknolojia mnazokuja nazo siyo tu za kisasa, bali ni zinazogusa maisha ya watu wa kawaida vijijini. Ni wajibu wetu sote kuhakikisha matokeo ya tafiti hizi yanawafikia walengwa kwa wakati,” alisema Mhe. Pinda.

Mhe. Pinda ni mgeni wa kudumu anayependa kutembelea banda la SUA kila mwaka katika Maonesho ya Nanenane, na ameendelea kuonyesha moyo wa kuunga mkono juhudi za taasisi hiyo katika kuendeleza sekta ya kilimo nchini.