KOCHA Mkuu wa Taifa Stars, Hemed Suleiman ‘Morocco’, amesema ushindi wa kwanza wa timu hiyo wa michuano ya CHAN umetoa mwanga mkubwa wa kikosi hicho kufanya vizuri zaidi.
Kauli ya Morocco, inajiri baada ya timu hiyo kuanza vyema michuano ya CHAN kufuatia kuifunga Burkina Faso mabao 2-0, katika mechi ya kwanza ya ufunguzi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.
“Narudia kusema tena mwaka huu tuna kikosi kizuri na bora ambacho naamini kinaweza kutufikisha hatua za mbali zaidi ya tunavyotarajia,” amesema.
Aidha Morocco amesema licha ya jinamizi la timu hiyo kutofanya vizuri katika michuano iliyopita, ila mwaka huu utakuwa ni wa tofauti zaidi kwa sababu ya jitihada zinazoonyeshwa na wachezaji.
“Ni kweli tumekuwa tunafanya vibaya sana na tulikuwa tunaishia hatua za makundi pekee, ila nafikiri sio muda wa kuangalia hilo kwa sababu hii ni michuano mingine na isitoshe pia tupo nyumbani,” amesema.