LICHA ya mashabiki waliojitokeza kwa wingi nje ya Uwanja wa Mkapa hali kwa wafanyabiashara sio nzuri baada ya kulalamikia biashara kutokwenda kama matarajio yao.
Nyomi iliyojitokeza hapa ikisubiri muda wa kuruhusiwa kuingia ndani wengi wamekuwa wakizunguka zunguka kuvuta muda huku wengine wakijipumzisha maeneo ya vivuli.
Wakizungumza na Mwanaspoti, wafanyabiashara waliopo nje ya Uwanja wa Mkapa wamesema hakuna amshaamsha kama kukiwa na mechi za Simba na Yanga.
“Nauza chakula gharama imeongezwa kidogo tofauti na siku za kawaida ambapo tunauza sahani ya wali shilingi elfu mbili sasa tumeongeza mia tano na sodo elfu moja siku za kawaida mia saba,” amesema muuzaji aliyejitambulisha kwa jina la mama Zaynab na kuongeza:
“Matarajio yalikuwa makubwa salakini hadi sasa muda umeenda saa kumi chakula bado kipo tofauti na tulivyozoea nafikiri mashabiki watakuwa wametoka majumbani mwao wamekula.”
Hassan Hamis ambaye ni muuza chips amesema biashara yao wanaifanya kama kawaida kwa bei ileile, lakini changamoto ni kukosa wateja lakini wanaamini bado wana nafasu ya kuuza kutokana na muda wa mechi uliopangwa.
“Tumefungua hapa kuanzia saa tano asubuhi biashara haijachangamka sana tofauti na tulivyozoea hasa mechi za watani Simba na Yanga,” amesema.