WADAU wa soka wa Kanda ya Pwani nchini Kenya wamezungumzia juu ya kiungo wa Harambee Stars, Mohamed Bajaber kuondoka katika kambi ya timu hiyo kwenda kujiunga na klabu yake mpya ya Simba ya Tanzania.
Bajaber amesajiliwa na moja ya wababe wa Ligi Kuu Tanzania, Simba ambayo wakati huu iko Ismaili nchini Misri ambako imepiga kambi kujiandaa kwa msimu mpya wa 2024-2025.
Mkurugenzi wa Ufundi wa Cosmos FC, Aref Baghazally amesema kuondoka kwa Bajaber kumeacha pengo kubwa ambalo haliwezi kuzibika Harambee Stars inayoshiriki mashindano ya CHAN.
“Kiuhakika Stars itamkosa mwanasoka huyu ambaye angelitoa mchango mkubwa, lakini pia hatufai kumlaumu kwa sababu klabu yake mpya ya Simba inamhitaji kwa ajili ya kuwa na wachezaji wenzake kujiandaa kwa msimu mpya,” amesema Baghazally.
Mwenyekiti wa FKF tawi la Mombasa, Alamin Ahmed amesema kocha wa timu ya taifa ya Kenya, Benny McCarthy amemchukulia Bajaber kuwa mchezaji aliyemtegemea kuwa katika kikosi na alimuamini.
“Lakini kwa upande mwingine, kuondoka kwa mwanasoka huyo kujiunga na Simba ni jambo la busara kwani litawapa chipukizi changamoto ya kufanya bidii na kuinua vipaji vyao na kuwa na malengo ya kucheza soka la kulipwa,” akasema Alamin.
Aliyekuwa mchezaji wa klabu iliyokuwa maarufu zamani ya Mwenge, Omar Faraj amesema kukosekana kwa Bajaber Harambee Stars ni pigo, lakini pia kumetoa nafasi yake kwa mchezaji mwingine kuonyesha kipaji chake kwenye mashindano ya CHAN.
“Tayari Bajaber ameonyesha ubora wake ndipo McCarthy akamuamini kumuweka kwenye kikosi chake cha kwanza. Lakini ni vizuri amekwenda kwenye timu bora Tanzania ataonekana kirahisi kufikia lengo lake la kucheza soka huko Ulaya,” amesema Faraj.
Naye kocha anyesimamia timu ya vijana ya Hamburg FC, Omar Batistita amesema Bajaber amefanya uamuzi mzuri kwenda Simba kwani malipo ya timu za Tanzania ni mazuri kuliko Kenya.
“Mwanasoka wetu huyo atakuja kuwakilisha Kenya kwenye mashindano mengine ya kimataifa, lakini hivi sasa amechukua uamuzi bora wa kuendeleza kipaji chake na kuwapa motisha vijana wengine wafuate mfano wake,” amesema Batistuta.
Bajaber amesajiliwa na Simba kutoka klabu bingwa ya Ligi Kuu Kenya, Kenya Police na pia aliwahi kuichezea Nairobi City Stars.