Watoto hawa hatarini kupata utapiamlo, tatizo liko hapa

Shinyanga. Watoto wasionyonyeshwa kikamilifu kwa miezi sita na wanaoanzishiwa vyakula mbadala mapema, wapo katika hatari ya kupata tatizo la utapiamlo, wataalamu wa afya wameonya.

Imeelezwa kuwa hali hiyo inaweza kuchangia mtoto kupata utapiamlo, hii moja kwa moja inasababishwa na ulaji usiofaa na magonjwa yanayompata mtoto.

Takwimu za Wizara ya Afya zinaonyesha asilimia 86 ya watoto wote nchini, huachishwa kunyonya miezi 15 baada ya kuzaliwa, sawa na umri wa mwaka mmoja na miezi mitatu, huku wakitaja athari zinazoweza kumkumba mtoto hapo baadae.

Hata hivyo asilimia 35 pekee ya watoto wote nchini, hunyonyeshwa kwa kipindi chote cha miaka miwili.

Tanzania kiwango cha ukondefu kwa watoto chini ya miaka mitano ni asilimia 3,  sawa na watoto 620,000 kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022.

Katika mkoa wa Shinyanga, baadhi ya wazazi wamezungumza sababu za kuanza kuwapa watoto chakula mapema, wakitaja sababu za utafutaji wa maisha hali inayowafanya washindwe kufuata kanuni sahihi za unyonyeshaji.

Wakizungumza na Mwananchi Digital leo Jumamosi Agosti 2, 2025 katika maeneo tofauti tofauti, mama wa watoto watatu Julieth Said ameeleza kuwa kutokana na harakati za utafutaji ilisababisha kuanza kumpa mtoto chakula akiwa na miezi mitatu tu.

“Shughuli za utafutaji katika biashara yangu ndio zilisababisha kuanza kumpa mtoto chakula mapema, kwa sababu sikuweza kuzunguka nae katika utafutaji, ilibidi aanze kula mapema ili nipate muda wa kutafuta pesa,” amesema Julieth.

“Ilikuwa ni ngumu kwangu kukaa miezi sita ukimtegemea tu mwanaume, muda mwingine akienda katika kazi yake anaweza kuja na kidogo, kukigawa mara mbili kwa wanafamilia na mimi mzazi unakuta haitoshi, kwa mantiki hiyo ilinibidi nimpe mtoto chakula kabla ya wakati ili azoee haraka nipate muda wa kufanya biashara huku nikimwacha nyumbani,” amesema Aisha Ramadhani.

Ili kuondokana na tatizo hili, Wizara ya Afya imezindua Mwongozo wa Kitaifa wa kuzuia na kutibu ukondefu, na uvimbe unaotokana na ukondefu kwa watoto walio na umri chini ya miaka mitano, hali iliyotajwa kusababishwa na unyonyeshaji duni na lishe isiyokidhi mahitaji kwa kundi hilo.

Ofisa lishe kutoka Hospitali ya Manispaa ya Shinyanga, Amani Mwakipesile ameeleza athari anazoweza kuzipata mtoto endapo hatonyonyeshwa ipasavyo na kuanza kupewa chakula kwa muda usioshauriwa.

“Mtoto kama hatonyonya inavyoshauriwa atapata utapiamlo, hii moja kwa moja inasababishwa na ulaji usiofaa na magonjwa yanayokuwa yanampata mtoto, pia anapofikisha miezi sita ndipo mzazi anaruhusiwa kumuanzishia chakula laini na kadri anavyozidi kukua ndipo unapoongeza ugumu wa chakula,” amesema Mwakipesile.

Ofisa Lishe kutoka Wizara ya Afya, Elieth Rumanyika amesema, mtoto asiponyonya kwa usahihi inaweza kuathiri ukuaji wake wa ubongo, atapata upungufu wa virurubisho muhimu mwilini ambavyo kusaidia ukuaji, itaathiri afya na serikali itatumia fedha nyingi kuwekeza kwenye afya.

“Mtoto ni Taifa la kesho, tusipowekeza tutakuwa na Taifa ambalo halina nguvu kazi, haliwezi kuzalisha na hivyo uchumi wetu utaporomoka kwa sababu hatuna uwezo wa kuzalisha, kufikiri, kujenga vitu na kubuni vitu vikubwa kwa ajili ya maendeleo ya nchi,” amesema Elieth.

Mikakati iliyowekwa kuzuia utapiamlo

Pia ameongeza, “Katika suala la magonjwa yanayosabibisha utapiamlo Serikali imeweka miundombinu wezeshi na kufanya matibabu ya bure kwa watoto, vifaa na dawa za kutosha katika hospitali zetu.”

“Kwenye tatizo la ulaji usiofaa au kula chakula kidogo hii inatengenezwa na jamii yetu, katika wiki hii ya unyonyeshaji tunaitumia kwa wanajamii kuwafundisha namna bora ya kuwalisha watoto wetu, tunawafundisha wazazi kutengeneza chakula chenye virutubisho kinachopatikana katika mazingira wanayoishi,” amesema Mwakipesile.

Ushauri wa wadau wa malezi na makuzi ya mtoto

Kuna tabia ambayo inachangia mtoto anayenyonya kutopata haki yake ya kunyonya kwa wakati anaostahili, ambayo inaweza kutafsiriwa kama kumfanyia mtoto ukatili, hii ni endapo mama atashindwa kumnyonyesha mtoto kwa kutokewa na uelewa,

“Hii mara nyingi hutokea kwa mabinti ambao wanaona aibu kuwanyonyesha watoto wao mbele ya watu bila kujua ni kumfanyia mtoto ukatili, kwa sababu hanyonyeshwi kwa wakati anapohitaji,” amesema Mariam Shabani.

“Katika tamaduni zetu mwanamke anatakiwa ajistiri ili kujijengea heshima kwa watu, tukija katika suala la kunyonyesha hicho ni chakula cha mtoto popote mama alipo anatakiwa kumnyonyesha mtoto lakini, tunashauri wakimama kutembea na nguo ya ziada kama kitenge ambacho kitakachotumika kujifunika wakati wa kunyonyesha katika mazingira ya wazi,” amesema Aghata Masaganya.

Kauli za viongozi wa dini

Mwenyekiti wa jumuiya ya maridhiano mkoa wa Shinyanga Sheikh Hamis Balilusa kwa upande wa dini ya Kiislamu ameeleza kuwa mzazi anatakiwa kuangalia ni vazi gani alilovaa litakalo mruhusu kumnyonyesha mtoto sehemu za wazi, kunyonya ni haki yake hadi atakapo fikisha miaka miwili kama mzazi hana tatizo la kiafya.

“Mzazi anatakiwa kuangalia nguo anayovaa ili kuepuka kujinajisi au kuonesha maungo yake wakati wa kunyonyesha, katika dini ya kiislamu mwanamke hatakiwi kuonyesha sehemu yoyote ya mwili isipokuwa kwa mumewe, hivyo ili kuwa na stala lazima atembee na mtandio mkubwa ili kujikinga na kuonyesha mwili wake na pia kutimiza hitaji la mtoto,” amesema Shekh.

Pia ameongeza, “Mzazi aliyehangaika na mtoto tumboni kwa miezi tisa akikumbuka taabu alizopita hutamani mwanawe awe na afya bora, hata dini pia tunashauri mtoto anyonye hadi miaka miwili itakayomsaidia kuwa na afya ya mwili na akili,” amesema Shekh Balilusa.