Watumishi majumbani wapaza sauti kilio cha haki

Dodoma. Wafanyakazi wa majumbani wamepaza sauti wakitaka kupewa haki zao za msingi za likizo ya mwaka, ugonjwa na ya uzazi kama ilivyo kwa kada nyingine za kazi nchini.

Vilevile wanataka haki ya kuwa na muda maalumu wa kufanya kazi na kupumzika kwa kuwa waajiri wengi hawatoi nafasi kwao ya kupumzika, hivyo hujikuta wakifanya kazi zaidi ya saa 12 hali inayosababisha kuchoka mwili na akili.

Pia, wametaka waajiri kuwalipa mshahara kwa wakati na kulingana na makubaliano waliyoingia.

Madai hayo wameyatoa leo Jumamosi Agosti 2, 2025 kwenye kikao kazi cha kuimarisha uelewa wa sheria za kazi, haki na wajibu kwa wafanyakazi wa majumbani kilichoandaliwa na Chama cha Wafanyakazi wa Mahotelini na Majumbani (Chodawu) jijini Dodoma.

Mariam Juma, amesema baadhi ya waajiri hawataki wafanyakazi wao wa nyumbani wapumzike hata kwa saa moja kwa siku.

“Tunataka haki yetu ya kupumzika hata saa moja kwa siku ili kuupa mwili nguvu. Baadhi ya waajiri wanataka tufanye kazi saa 12 na kuna wengine wanafanya kazi zaidi ya hapo, wanawahi kuamka na wanachelewa kulala kila siku,” amesema.

Nuruel Zawadi amesema waajiri wengi hawataki kutoa mikataba ya kazi kwa wafanyakazi wa nyumbani, hivyo inakuwa vigumu kudai haki pale zinapokiukwa kwa kuwa hakuna mkataba wa kuwalinda.

“Imefika hatua ukiumwa, ukibeba mimba au hata ukifiwa ndiyo inakuwa mwisho wako wa kazi, lakini tunaona kwenye kada nyingine wafanyakazi wanakwenda likizo za uzazi, likizo za ugonjwa na za mwaka, baada ya hapo wanarudi kuendelea na kazi, na sisi tunataka hivyo,” amesema.

Katibu Mkuu wa Chodawu, Selemani Wamba amewataka wafanyakazi wa majumbani kutimiza wajibu wao wa kufanya kazi kwa bidii kwani hakuna haki bila wajibu.

Amesema kuna baadhi ya wafanyakazi wa majumbani wakishapata kazi wanajisahau, badala ya kufanya kazi wanakuwa wavivu.

Ofisa kutoka Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA), Halima Suleimani amewataka wafanyakazi wa majumbani kuingia mikataba ya kazi na waajiri ili iwe rahisi kupata haki zao pale zinapokiukwa.

Amesema mikataba ndiyo silaha pekee ya kuwasaidia kufanya kazi kwa uhuru na utulivu kwa kuwa majukumu yote ya kazi yanaingizwa humo ili yatakapokiukwa hatua za kisheria zichukuliwe kwa upande wa mwajiri na mwajiriwa.

“Msing’ang’anie kwenye haki pekee lakini pia timizeni wajibu wenu unaowapeleka kufanya kazi za nyumbani kama vile kufanya usafi, kulea watoto na wazee na kuhakikisha nyumba za waajiri wenu zinakuwa salama. Mkifanya hayo yote sasa ndipo mdai haki zenu za likizo na mshahara kwa wakati,” amesema.

Mratibu wa mradi wa kuwajengea uwezo wafanyakazi wa majumbani, Chiku Semfuko amesema mafunzo hayo yanalenga kuwakumbusha wafanyakazi wa majumbani haki na wajibu wao wanapotekeleza shughuli zao za kila siku.

Amesema kumekuwa na vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa wafanyakazi wa majumbani hali inayosababisha vifo, unyanyasaji wa kingono, matusi na kipigo jambo ambalo halikubaliki kisheria.

Amesema mafunzo hayo yatawajengea uwezo wa kujua haki, wajibu na uelewa wa sheria za kazi kwa wafanyakazi wa majumbani ili watakapokutana na changamoto wajue mahali pa kupeleka malalamiko yao.