WANARIADHa 5000 kutoka ndani na nje ya nchi wanatarajia kuchuana katika mbio za kimataifa za Mwalimu Julius Nyerere zinazotarajia kufanyika jijini Mbeya.
Mbio hizo zinazoandaliwa na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) kwa kushirikiana na ofisi ya Waziri Mkuu ni msimu wa pili kufanyika baada ya mwaka jana kurindima jijini Mwanza na sasa ni Mbeya.
Akizungumza jana kwa niaba ya Mkurugenzi wa Shirika hilo, Dk Ayoub RiobaRioba, Mkurugenzi wa Habari na Matukio, Eshe Muhidini amesema mbio hizo zinatarajia kufanyika Oktoba 11 zikifuatiwa na matukio mengine kadhaa.
Eshe amesema katika mbio hizo, kutatanguliwa na matukio mengine ikiwamo Insha kwa Wanafunzi, mdahalo utakaombatana na kilele cha wiki ya vijana na uzimaji mwenge kitaifa akibainisha kuwa tukio hilo ni kufanya kumbukizi ya kifo cha Hayati Mwalimu Julius Nyerere.
“Mbio hizi kwa mwaka huu zitashirikisha washiriki kutoka nje ambapo matarajio ni watu 5,000 watakaokimbia mbio hizi, ada ya mshiriki ni Sh 25,000,” amesema Eshe.
Ameongeza lengo la mbio hizo ni kuwasaidia makundi maalumu upande wa ulemavu pamoja na kujenga uhusiano, kuimarisha afya na kuhamasisha amani, upendo na utulivu kwa kipindi hiki cha uchaguzi.
“Zoezi la usajili litaanza Agosti 15 katika vituo tofauti ikiwamo ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya na itakuwa kidigitali, kuhusu zawadi tutaingaza baadaye japokuwa medali zitakuwapo kwa washiriki,” amesema Mkurugenzi huyo.
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Beno Malisa amesema mbio hizo ni fursa kubwa kwa wakazi wa Mkoa huo pamoja kanda nzima ya Nyanda za Juu Kusini akiwaomba wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki mbio hizo.
Amesema katika mbio hizo zitakimbiwa viwanja vya Sokoine, zitashirikisha kilomita tano, 10 na 21 na kwamba Mkoa huo umejipanga kufanikisha shughuli hiyo kubwa nchini.
“Hii ni fursa kubwa kwa ukanda wetu Nyanda za Juu Kusini, tunasisitiza amani na utulivu, swala la zawadi zitatangazwa kwakuwa ni mbio za ushindani, japokuwa kutakuwapo na Insha kwa Wanafunzi wa Sekondari ambapo kwa sasa yanaendelea hapa nchini,” amesema Malisa.
Mratibu wa matukio TBC, Anna Mwasyoke amesema kwa sasa wanaendelea kufanya mawasiliano kujua watakaonogesha tukio hilo akieleza kuwa mara kadhaa hushirikisha makundi ya Jogging.
“Tunaendelea kuratibu kuhusu wale watu maarufu watakaotumbuiza na kunogesha tukio, japo tumekuwa tukishirikisha makundi ya Jogging hivyo tunaendelea kushirikiana na kamati na tutakuwa tunawajulisha,” amesema Anna.