Mwanza. Benki ya NMB imekutana na wafanyabiashara wakubwa 120 wa Mkoa wa Mwanza na kuwahakikishia uwezo wa kupata mikopo mikubwa.
Akizungumza na wafanyabiashara katika hafla ya chakula cha usiku Agosti 1,2025 jijini Mwanza, Ofisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara wa NMB, Filbert Mponzi amesema benki hiyo ina uwezo wa kuwahudumia wafanyabiashara nchini kwa kutoa mkopo wa hadi Sh 550 bilioni kwa mteja mmoja.
“Hii ni ishara tosha ya uimara wa NMB katika masuala ya fedha na uwezo wa kweli wa kuwahudumia wafanyabiashara wakubwa,” amesema Mponzi.
Ameipongeza Serikali kwa kuweka mazingira mazuri ya biashara, jambo alilosema limechangia ukuaji wa sekta binafsi na kuongeza uhitaji wa huduma za kifedha.
Mponzi amesisitiza kuwa, NMB iko tayari kutoa suluhisho kwa wafanyabiashara ikiwamo mikopo, mifumo ya malipo ya kisasa na huduma za bima.

“Tuna masuluhisho yote muhimu kwa wafanyabiashara. Tumejipanga vizuri kuwahudumia kuanzia mikopo, ubunifu wa malipo hadi bima ya mkono wa pole, hivyo msisite kuleta mahitaji yenu, sisi tupo kwa ajili yenu,” amesema Mponzi.
Akielezea mafanikio ya benki hiyo, amesema NMB imetambuliwa kama benki salama zaidi nchini kwa miaka mitatu mfululizo na Jarida la Global Banking & Finance na imeshinda tuzo ya benki bora Tanzania mara 11 katika miaka 13 iliyopita kutoka Jarida la Euromoney.
Mwenyekiti wa Wafanyabiashara Mkoa wa Mwanza, Gabriel Mgini ametoa shukrani kwa NMB kwa uaminifu na mshikamano waliouonesha kwa wateja wao, hata katika nyakati ngumu za biashara.
“Kwa niaba ya wafanyabiashara wenzangu, tunawashukuru sana kwa namna ambavyo mmekuwa karibu na sisi. Mmekuwa mstari wa mbele kutuvumilia, kutusikiliza na kutembea na sisi katika hatua zote za kibiashara kwenye mafanikio na changamoto,” amesema Mgini.
“Ni wazi kuwa, kwa mfanyabiashara ili apige hatua, lazima ashirikiane na benki imara. NMB imejidhihirisha ndiyo benki sahihi kwetu, licha ya uwepo wa benki nyingi nchini, huduma za NMB zimeendelea kuwa bora na za kuaminika.”
Mgini amewaahidi wafanyabiashara wa Mwanza kuendelea kuitumia Benki ya NMB kama mshirika wao wa karibu katika kukuza biashara.
Meneja wa NMB Kanda ya Ziwa, Faraja Ngingo amesema wafanyabiashara ni sehemu muhimu katika mafanikio ya benki hiyo na kwamba, haiwezi kufikia malengo yake bila kuwahusisha wateja wake kwa karibu.
“Tunatambua mchango wenu kwetu, benki yetu haiwezi kufanikiwa bila ninyi kuwepo, huduma yetu haiwezi kuwa ya thamani bila kuzingatia mahitaji yenu na kujitolea kwenu katika kuwahudumia,” amesema Faraja.
“Tunawashukuru kwa kuendelea kutuamini, kwa pamoja tutaendelea kujenga huduma zinazozingatia ubunifu, urahisi, unafuu na maadili. Tunathamini sana imani yenu, uaminifu na mchango wenu katika mafanikio yetu kama Benki ya NMB.”
“Tutaendelea kujitolea kwa ajili yenu na tunatazamia kuwa na uhusiano wa muda mrefu unaojengwa katika msingi wa kuheshimiana na kushirikiana,”amesema Faraja.
Hafla hiyo imewakutanisha viongozi waandamizi wa NMB, wawakilishi wa Serikali na wafanyabiashara.