Célestin Ecua atuma salamu nzito

SAA chache baada ya Célestin Ecua kutambulishwa kuwa mchezaji wa Yanga, mwenyewe ameibuka na kutuma ujumbe wenye ahadi ya kufanya vizuri zaidi kuipa mafanikio klabu hiyo ambayo msimu uliopita ilibeba mataji matano ambao ni Kombe la Toyota, Ngao ya Jamii, Kombe la Muungano, Ligi Kuu Bara na Kombe la FA.

Ecua ambaye ametua Yanga akitokea Zoman ya Ivory Coast, amesaini mkataba wa miaka mitatu kuwatumikia mabingwa hao wa kihistoria wa Ligi Kuu Bara.

Mshambuliaji huyo ambaye msimu uliopita alikuwa akiichezea Asec Mimosa kwa mkopo, ndiye Mchezaji Bora (MVP) wa Ligi Kuu ya Ivory Coast 2024-2025 kutokana na kufanya vizuri akihusika kwenye mabao 27 katika mechi 30 akifunga 15 na asisti 12, amesema atawafurahisha mashabiki wa Yanga na wale wote wanaomsapoti kwa lengo la kurudisha fadhila hizo.

“Kutoka chini ya moyo wangu nataka kutoa shukrani zangu za dhati kwa watu wote ambao wameniunga mkono hadi sasa. Kutia moyo, maombi na imani yao imekuwa nguvu yangu kufika hapa.

“Shukrani za pekee kwa familia yangu, marafiki, makocha na kila mtu ambaye aliniamini hata nilipokuwa katika wakati mgumu. Bila wao, hatua hii muhimu katika kazi yangu isingewezekana.

“Pia ninamshukuru Mungu, chanzo cha neema yote, kwa baraka na mwongozo wake wa kila mara.

“Leo, ninajivunia na kuheshimiwa kujiunga na Yanga SC, ninaahidi kufanya niwezavyo kuheshimu sapoti yenu.”

Wakati Ecua akituma ujumbe huo, kampuni ya uwakala inayosimamia madili yake, Wa Football Agency, ilisema: “Tunajivunia kutangaza rasmi mchezaji wetu Ecua Celestin amejiunga na klabu maarufu na ya kihistoria ya Tanzania, Yanga SC kwa mkataba wa misimu mitatu, mbele ya mwakilishi wa Wa Football Agency, Papida Tsava.

“Asante za dhati kwa Rais Hersi Said na wanachama wote wa klabu kwa weledi wao, uaminifu wao, na ushirikiano wao kukamilisha uhamisho huu.

“Tunamtakia mchezaji wetu mafanikio makubwa katika klabu hii. Mambo mazuri zaidi yanakuja MVP.”

Usajili wa Ecua unaenda kuongeza nguvu eneo la ushambuliaji la timu hiyo kwa kuungana na Prince Dube, Clement Mzize waliokuwepo hapo msimu uliopita. Pia Andy Bobwa Boyeli ambaye naye ni usajili mpya.

Msimu uliopita katika Ligi Kuu Bara, Mzize aliibuka kinara wa ufungaji kwa wachezaji wazawa akifunga mabao 14, huku Dube akifunga 13, matatu nyuma ya kinara Jean Charles Ahoua wa Simba, lakini pia sawa na Jonathan Sowah aliyekuwa Singida Black Stars na sasa amesaini Simba, Steven Mukwala (Simba) na Leonel Ateba (Simba).

Hadi kufikia jana mchana, Yanga katika maboresho ya kikosi chake kuelekea msimu ujao, ilikuwa imetambulisha wachezaji wapya saba ambao ni Balla Moussa Conté kutoka CS Sfaxien, Offen Chikola (Tabora United), Abdulnassir Mohamed Abdullah ‘Casemiro’ (Mlandege FC), Lassine Kouma (Stade Malien), Abubakar Nizar Othman ‘Ninju’ (JKU), Andy Bobwa Boyeli (Sekhukhune United FC) na Celestin Ecua (Zoman FC).

Mbali na hao pia imetangaza kuwaongezea mikataba nyota wake sita ambao ni Aziz Andabwile, Israel Mwenda, Maxi Nzengeli, Duke Abuya, Denis Nkane na Pacome Zouzoua.