Clara Luvanga, Chelsea kuna kitu

CHELSEA ambayo ni bingwa wa Ligi Kuu ya wanawake ya England, Chelsea imeelezwa imevutiwa na kiwango cha mshambuliaji wa Kitanzania, Clara Luvanga anayekipiga Al Nassr ya Saudi Arabia.

Tayari Luvanga ameichezea Al Nassr misimu miwili tangu aliposajiliwa mwaka 2023 akitokea Dux Logrono ya Hispania, aliyocheza kwa miezi mitatu tu na kupata shavu hilo.

Mmoja wa viongozi wa kampuni inayomsimamia Clara aliliambia Mwanaspoti Chelsea imefungua mazungumzo na mabingwa wa Ligi Kuu ya Saudia kumtaka mshambuliaji huyo wa timu ya taifa, Twiga Stars na tayari wameshapeleka ofa yao.

“Wamepeleka ofa ya kumtaka Clara na sasa inaangaliwa na timu anayoichezea kwa sababu bado ana mkataba nao wa mwaka mmoja. Kwa hiyo, viongozi wanaangalia ofa kubwa kutokana na upatikanaji wa washambuliaji wa aina yake,” alisema kiongozi huyo.

Msimu wake wa kwanza Al Nassr, alifunga mabao 11 na kutoa asisti saba na kuisaidia kutetea ubingwa wa ligi hiyo, huku uliopita aliweka kambani mabao 21 na asisti saba.

Kama Clara atasajiliwa na Chelsea, atakuwa mchezaji wa pili kuichezea Ligi Kuu England baada ya Aisha Masaka aliyesajiliwa na Brighton msimu uliopita akiwa ni Mtanzania wa kwanza kwa soka la wanawake, akicheza mechi mbili pekee kwa dakika 14, dhidi ya Arsenal na Birmingham.