Dosari zasababisha kesi ya ubakaji kwa genge kusikilizwa upya

Arusha. Mahakama Kuu Masjala Ndogo Bukoba imebatilisha na kufuta adhabu ya kifungo cha maisha jela waliyohukumiwa washtakiwa wawili baada ya kutiwa hatiani kwa ubakaji wa genge.

Uamuzi wa Mahakama umetokana na kubainika dosari za kisheria, huku ikiamuru kesi irejeshwe Mahakama ya chini na isikilizwe mbele ya hakimu mwingine mwenye mamlaka.

Pia imeamuru kuchunguza umri wa mrufani wa kwanza katika kesi hiyo ambaye kwenye rufaa alidai alihukumiwa akiwa na miaka 17.

Warufani hao ni Binemungu Robart na Hashimu Said ambao pamoja na mwenzao ambaye siyo mrufani katika rufaa hiyo walitiwa hatiani kwa kumbaka kwa genge binti wa miaka 15.

Tukio hilo lilidaiwa kutokea Novemba 4, 2024 katika Kijiji cha Ruhita wilayani Kyerwa, Mkoa wa Kagera.

Kwa mujibu wa hukumu, shtaka lilisomwa kwa msaada wa mkalimani na awali washtakiwa walikana kosa na baadaye ilidaiwa walikiri, lakini haionyeshi ni wapi hakimu aliwaeleza warufani kosa waliloshtakiwa nalo na haikuandikwa kuonyesha walikiri.

Dosari nyingine ni warufani kutopewa nafasi ya kupinga au kueleza ukweli wowote kwa kilichosomwa na upande wa mashtaka, hivyo kusababisha utata na haikuwa salama kutegemea katika kuwatia hatiani.

Hukumu hiyo imetolewa Julai 30, 2025 na Jaji Lilian Itemba aliyesikiliza rufaa hiyo ya jinai na nakala yake kuwekwa kwenye mtandao wa Mahakama.

Awali warufani (washtakiwa) walifikishwa Mahakama ya Wilaya ya Kyerwa kwa kosa la ubakaji wa genge kinyume cha kifungu cha 130 (1) (2) (e) na 131A (1) (2) (3) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu.

Novemba 18, 2024 walitiwa hatiani kwa kukiri kosa na kuhukumiwa adhabu ya kifungo cha maisha jela na viboko vinne, huku mshtakiwa wa tatu, Julian Robart aliyekuwa mtoto alihukumiwa kifungo cha miezi sita jela na kufanya usafi Kituo cha Polisi Mabira.

Hawakuridhika wakakata rufaa. Warufani hawakuwa na uwakilishi wa wakili, walipinga uamuzi huo kwa hoja nne kwamba, mahakama ilikosea kisheria kuwatia hatiani na kuwahukumu kwa kosa ambalo hawakuwahi kukiri.

Hoja nyingine ni madai ya kukiri kosa kuwa na utata kwani mahakama ya chini ilikosea kuchukulia kama ombi la hatia, hakimu alikosea kisheria kuwatia hatiani na kuwahukumu kwa kukiri makosa na kutokuelewa.

Binemungu alidai alitiwa hatiani kwa kosa hilo lakini hamfahamu mwathirika wa tukio hilo na hakufika mahakamani kutoa ushahidi, pia alikuwa na miaka 17 alipotiwa hatiani, hivyo alikuwa mtoto.

Upande wa Jamhuri uliwakilishwa na Wakili wa Serikali, Matilda Assey aliyeunga mkono rufaa.

Alieleza kwa kuangalia mwenendo wa kesi katika ukurasa wa pili, warufani waliwasilisha ombi la kutokuwa na hatia.

Alisema cha ajabu ukurasa wa tatu mahakama iliandika warufani walikiri, jambo ambalo halikuwa sahihi na kwamba, hata kama warufani wangekiri, kulipaswa kuainishwa vipengele walivyokubali na ambavyo hawakukubali.

Wakili huyo amesema kinyume chake, imeandikwa kuanzia namba moja hadi sita ukweli, bila ukweli huo kusemwa na kuwa baada ya warufani kuwasilisha ombi la kutokuwa na hatia, Mahakama ilitakiwa kupanga tarehe nyingine ambapo kesi hiyo ingeendelea kwa shahidi kuitwa.

Baada ya kurejea kesi inayoeleza utaratibu unaopaswa kufuatwa, alieleza usikilizwaji wa kesi Mahakama ya chini ulikuwa na dosari, hivyo Mahakama inapaswa kuamuru kesi kusikilizwa upya.

Kuhusu umri wa mrufani wa kwanza, aliwasilisha hoja kwamba iwapo kesi itarejeshwa Mahakama ya chini kwa ajili ya kusikilizwa ni muhimu hakimu kuchunguza umri wake kabla ya kesi kuanza.

Jaji Itemba amesema baada ya kuzingatia rekodi na mawasilisho ya pande zote mbili, ataangalia sababu za rufaa zilizowasilishwa na warufani kuungwa mkono na mjibu rufaa.

Jaji akinukuu sehemu ya kesi iliyokatiwa rufaa, amesema kumbukumbu za mahakama zinaonyesha shtaka lilisomwa na kuelezwa kwa washtakiwa kwa lugha wanayoielewa (Kinyambo).

Amesema sehemu hiyo inaeleza mshtakiwa wa kwanza na wa pili walikana kutenda kosa ila wa tatu (siyo mrufani) alikiri kosa.

Amesema Novemba 18, 2024 wakati wa usikilizwaji wa awali, warufani na mwenzao wa tatu walisomewa majina yao, anwani zao na kosa walilotenda, ambapo wakiwa Kituo cha Polisi cha Mabira waliandika maelezo  ya onyo na kukiri kufanya kosa hilo na walipofikishwa mahakamani walikana.

Jaji amesema katika kumbukumbu inaonyesha washtakiwa walikubali mambo yote sita waliyosomewa kupitia mkalimani licha ya wakati shtaka likisomwa walikana kutenda, isipokuwa aliyekuwa mshtakiwa wa tatu.

“Hitilafu hii inadhoofisha tu uhalali wa hatia, kuhusu vielelezo vinavyodaiwa kama vile maelezo yaliyoonywa, haionyeshwi kama vilikubaliwa ipasavyo na kama vilisomwa mbele ya warufani,” amesema na kuongeza:

“Zaidi ya hayo, kama ilivyoelezwa kwa usahihi na wakili wa Serikali, hata kama mrufani angekubali kukiri kuwa na hatia kuna hati iliyothibitishwa utaratibu utakaofuatwa na mahakama baada ya ombi hilo.”

Jaji Itemba amesema sheria imeeleza rufaa juu ya pingamizi la hatia inaweza tu kuruhusiwa ikiwa ombi hilo halikuwa kamili, lenye utata au halijakamilika na kwa sababu hiyo, mahakama ya chini ilikosea kisheria katika kulichukulia kama ombi la hatia.

Nyingine ni kwamba, alikiri hatia kwa sababu ya makosa au kutoelewa na sababu ya tatu ni shtaka halikufichua kosa lolote linalojulikana na sheria au mrufani kushinikizwa kukiri au ombi la hatia kupatikana kutokana na tishio.

Jaji Itemba alinukuu kesi mbalimbali za rufaa kuhusu mazingira ya kesi ya namna hiyo na kueleza katika rufaa hiyo inaonekana shtaka hilo lililosomwa kwa msaada wa mkalimani, warufani walikana kutenda kosa hilo.

“Waliposomewa maelezo ya awali walikiri hatia, hakuna uthabiti, kwa hivyo ombi hilo si kamilifu na lina utata. Haionyeshwi ni wapi hakimu anamweleza mshtakiwa viungo vyote vya kosa aliloshitakiwa na mshitakiwa akikubali mambo hayo yote muhimu,” amesema.

Jaji amesema: “Haijaandikwa kama walisema kukiri ukweli huo au kama walisema chochote kwa maneno yao wenyewe. Warufani hawakupewa nafasi ya kupinga au kueleza ukweli wowote kufuatia ukweli uliokuwa ukisomwa na mwendesha mashtaka.”

Amesema hakuna taarifa za ukweli za jibu la warufani zaidi ilikuwa ni rekodi ya jumla kukiri ukweli bila kueleza ukweli huo, hivyo Mahakama imekubali rufaa hiyo na imebatilisha na kufuta hukumu iliyotolewa na mahakama ya wilaya.

Amesema kwa masilahi ya haki, jalada la kesi lirudishwe katika mahakama hiyo kwa ajili ya usikilizwaji mbele ya hakimu mwingine mwenye mamlaka.

Pia ameamuru Mahakama kuchunguza umri sahihi wa mrufani wa kwanza wakati wa usikilizwaji ili kubaini ni mtoto au la.