Musoma. Wakazi wa Kijiji cha Nyang’oma wilayani Musoma, Mkoa wa Mara, wameiomba Serikali kuingilia kati na kuwaondoa fisi na nyani ambao wamekuwa kero na tishio kijijini hapo.
Wakazi hao wamedai kuwa maisha yao yapo hatarini kutokana na kukithiri kwa fisi na nyani ambao wamekuwa wakiingia kijijini hapo na kuleta usumbufu, huku wakiwa hawajui nini cha kufanya.
Wakizungumza kijijini hapo jana, Jumamosi, Agosti 2, 2024, wakazi hao wamedai hivi sasa wanaishi kwa hofu ya kuuawa na wanyama hao kutokana na kushindwa kuwadhibiti ili wasiweze kuingia kijijini hapo.
Wamesema fisi wamekuwa wakisababisha madhara makubwa hasa kwa mifugo yao, ambapo wamekuwa wakiua mifugo na kuila, huku binadamu nao wakijeruhiwa.
“Kwa sasa hakuna mtu aliyeuawa, ila kwa hali inayoendelea si ajabu tukaanza sasa kuuawa na wanyama hawa. Wamekuwa wakivamia kwenye miji, ambapo wanakula mifugo na kusababisha hasara na ukitaka kupambana nao wanakujeruhi,” amesema Mirumbe John.
Nyarugumba Emmanuel amesema fisi hao wanaishi katika mapango yaliyopo kijijini hapo, huku akiiomba Serikali kuangalia namna ya kufukia mapango hayo ili yasiendelee kuwa makazi ya fisi.

“Fisi wanabomoa mabanda na kula mifugo. Mimi jana wamebomoa banda langu na kula mbuzi wawili, na watoto wanapoenda shuleni wanakutana nao, hivyo wanajikuta wakikimbia kila mmoja kwa uelekeo wake, wengine wanaumia na wengine wanajikuta wamepoteza uelekeo kabisa,” amesema.
Amesema uwepo wa wanyama hao kijijini hapo, mbali na kuwa kero na kuwasababishia hasara, pia kumesababisha washindwe kufanya shughuli za kimaendeleo kikamilifu kama ilivyokuwa awali kabla ya uwepo wa wanyama hao.
“Kwa sasa tunaogopa kuamka asubuhi kuwahi kwenye shughuli zetu, badala yake tunasubiri kupambazuke zaidi, na pia tunaogopa kutembea mmoja mmoja, kwa hiyo tunalazimika kutembea kwa makundi,” amesema.
Nyanjiga Mujungu amesema fisi hao wamekuwa na kawaida ya kuingia kijijini hapo saa 12 jioni na kufanya uharibifu kwenye miji kabla ya kurudi kwenye makazi yao asubuhi ya siku inayofuata.
“Sasa hivi hata watoto inabidi tuwasindikize hadi shuleni na kuwafuata, na wakati huo ukiwa umetoka unawaza nyumbani pakivamiwa hali itakuwaje. Kwa kweli hii ni kero kubwa na tuna hofu sana, tunaomba msaada wa haraka,” amesema.
Amesema katika mazingira kama hayo hakuna shughuli yoyote ya maendeleo inayoweza kufanyika, zaidi ya wakazi kuwa na hofu ya kuuawa au kujeruhiwa na wanyama hao muda wowote.
“Kwa sasa wanaingia kijijini jioni na kuondoka asubuhi, lakini kadri muda unavyokwenda wanaweza kuanza kuingia muda wowote na hii itakuwa hatari zaidi, tunaomba msaada wa haraka kabla hali haijawa mbaya,” amesema Fikiri Masinde.
Amesema miongoni mwa shughuli zilizoshindwa kufanyika kwa wakati huu ni pamoja na kilimo, ambapo wanaogopa kuwahi kwenda mashambani, huku wanawake pia wakishindwa kwenda ziwani kuchota maji kwa ajili ya matumizi ya nyumbani kwa kuhofia kukutana na fisi.
Kuhusu nyani, wakazi hao wamesema wanyama hao pia wamekuwa na tabia ya kuvamia miji na kula vyakula vilivyopo, huku wengine wakiondoka na kuku na bata kutoka kwenye miji waliyovamia.
“Hapa kwangu nyani aliuwa mbwa na kuingia ndani akala chakula, kisha akabeba kuku na kuondoka naye, kwa kweli hali sio nzuri,” amesema Mjarifu Mnyaki.
Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Juma Chikoka, amekiri kuwepo kwa hali hiyo kijijini hapo na kwamba tayari hatua zimeanza kuchukuliwa.
Amesema hatua zilizochukuliwa ni pamoja na ofisi yake kuagiza Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Pori (Tawa) kufika kijijini hapo mara moja ili kushughulikia suala hilo kwa haraka kabla hali haijawa mbaya.
“Ni kweli kuna hali hiyo pale kijijini, lakini hivi tunavyoongea tayari nimewaagiza Tawa wafike pale na kuchukua hatua ili kuwanusuru wakazi wale na kadhia hiyo, kwani Serikali pamoja na mambo mengine ina jukumu la kulinda usalama wa raia na mali zao,” amesema Chikoka.