GARI maalumu kwa ajili ya mashindano ya dunia (World Rally Championship) linatarajiwa kuwa kivutio kikubwa katika raundi ya tatu ya mbio za ubingwa wa Taifa zitakazochezwa Morogoro hivi karibuni.
Dereva kutoka Iringa, Ahmed Huwel ndiye ataendesha gari hilo, Toyota GR Yaris ambalo ni ingizo la kisasa zaidi katika raundi hii inayobeba bango la Mkwawa Rally of Morogoro.
Huwel alilinunua gari hilo kutoka kwa mshiriki wa mbio za magari ya dunia (WRC) kutoka Ubelgiji, Stephane Lefebvre.
“Litakuwa ni gari la pekee katika mashindano ya dunia kushiriki mbio za Mkwawa. Uwepo wake unazidi kupandisha hadhi ya raundi hii ya mbio za ubingwa wa Taifa,” alisema Mwenyekiti wa klabu ya Mount Uluguru, Gwakisa Mahigi.
Kwa kuingia na Toyota GR Yaris, Huwel itabidi aliweke pembeni gari aina ya Ford Fiesta Proto, ambalo amekuwa akilitumia kwa zaidi ya muongo mmoja sasa.
Hadi kufikia mwishoni mwa juma, orodha ya madereva waliojiandikisha ilifikia watu 17 baada ya Kelvin Taylor kuongezeka wikiendi iliyopita.
Toyota GR Yaris ndiyo magari yanayotamba katika mbio za magari ubingwa wa dunia na hii ilidhihirika Kenya katika mashindano yaliyofanyika mwezi Aprill baada ya kuchukua nafasi ya kwanza na ya pili licha kutawala 10 bora ya mashindano hayo.
Raundi ya tatu ya mbio za magari za Mount Uluguru imechukua jina shujaa wa Wahehe na kutambulika rasmi kama Mkwawa Rally of Morogoro. Itachewa Agosti 16 na 17 mwaka huu mkoani Morogoro.