INEC yaonya wazalishaji maudhui mitandaoni kuitumia ‘AI’ kupotosha

Dar es Salaam. Wazalishaji maudhui ya mtandaoni nchini Tanzania wametakiwa kuripoti taarifa za ukweli na uhakika katika majukwaa ya mitandao ya kijamii wakati Taifa likielekea kwenye Uchaguzi Mkuu wa madiwani, wabunge na Rais Jumatano ya Oktoba 29, 2025.

Sambamba na hilo, wametakiwa kuepuka matumizi mabaya ya Akili Unde (AI), ambayo baadhi ya watu wanatumia kusambaza taarifa za upotoshaji katika kuzalisha maudhui hayo.

Rai hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa INEC, Jaji Jacobs Mwambegele leo Jumapili Agosti 3, 2025 wakati akifungua mkutano wa kitaifa wa tume hiyo na wazalishaji maudhui mtandaoni kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

Ikumbukwe Akili Unde ni teknolojia inayowezesha kompyuta na mashine kuiga uwezo wa binadamu kama vile kujifunza, kufikiri, kufanya uamuzi, na kuwa na ubunifu. Katika sekta mbalimbali kama afya, elimu, fedha, masoko, na mawasiliano.


Miongoni mwa zana za Akili Unde kama Google AI Studio, ChatGPT, SORA (OpenAI), VEO, Gemini (Google), zinasaidia kurahisisha kazi, kuchambua data, na kuimarisha uamuzi wa kibiashara au binafsi au hata kufundishia.

Aidha kuna teknolojia za kisasa kama Deepfake zinahusisha picha, video au sauti zinazozalishwa na AI, za kweli lakini za kubuni ambazo hudhibiti maudhui yaliyopo au kuunda maudhui mapya kabisa.

Akizungumza Jaji Mwambegele amesema mitandao ya kijamii imekuwa chanzo muhimu ya habari na elimu kwa kuwa taarifa zinazosambazwa kwenye mitandao zinapatikana kwa urahisi na haraka.

“Hivyo natoa wito kwamba taarifa mnazoziweka kwenye mitandao yenu ni za ukweli na zisizo na chembe ya upotoshaji kwani ukosefu wa umakini kwenye eneo hili, unaweza kuharibu na kuvuruga kabisa amani na utulivu wa nchi.

“Pia nawasisitiza na kuwakumbusha juu ya umuhimu wa kuepuka matumizi mabaya ya AI, ambayo inatumiwa na baadhi ya watu wenye nia ovu kusambaza habari za upotoshaji kupitia mitandao hasa ya kijamii,” amesisitiza Mwenyekiti huyo.

Amesema Tume inatarajia wazalishaji maudhui kutoa maudhui yenye kuelimisha jamii na kuondoa upotoshaji ambao umekuwa ukitolewa mitandaoni.

Awali, akieleza zaidi Jaji Mwambegele amesema wazalishaji mtandaoni wanatambuliwa kama daraja la mawasiliano na wadau muhimu wa uchaguzi.

Akifafanua zaidi Ramadhani Kailima, Mkurugenzi wa Uchaguzi INEC, katika mkutano huo ambao ni mwendelezo wa vikao na makundi mbalimbali, amesema makosa yeyote yanayohusiana na mtandao yatashughulikiwa kisheria.

“Tumieni AI, kwa uangalifu msije kuharibu amani ya nchi mkitumia vibaya ipo sheria ambayo itakukamata,” amesema Kailima.

Akizungumza alipotafutwa na Mwananchi Mkurugenzi Kampuni ya Tehama ya Serensic Africa, Esther Mengi amesema AI imekuwa nyenzo yenye nguvu kwa wazalishaji maudhui katika kuandika, kutengeneza video, sauti na picha.

Amesema wakati wa uchaguzi, AI inaweza kutumiwa vibaya kwa mfano matumizi ya Deepfakes katika kutengeneza video/sauti feki za wagombea. Taarifa potofu, kusambaza habari za uongo haraka.

Esther ambaye ni mtaalamu wa masuala ya usalama mtandaoni amesema kwa namna INEC wanavyogusia basi inaonesha wanaelewa changamoto hizi mpya za teknolojia.

 “Kuna haja ya ushirikiano kati ya INEC, wazalishaji, vyombo vya habari na majukwaa ya kidijitali ili kudhibiti matumizi mabaya ya AI,” amesema.

Naye Mhadhiri Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA), kampasi ya Songea, Dk Bakari Mashaka amesema wanaweza kuitumia kuzalisha maudhui ya mada mbalimbali.

“Pia kuitumia kuwaelezea wagombea na sifa zao. Lakini pia wanaweza kuitumia kupata mwelekeo wa matokeo kutokana na mwenendo wa uchaguzi,” amesema.