UONGOZI wa Coastal Union unadaiwa kufikia hatua nzuri ya kuinasa saini ya aliyekuwa kiungo wa Geita Gold, Ally Ramadhan Kagawa akiwa mchezaji huru baada ya kumaliza mkataba na waajiri wake wa zamani.
Kagawa amemaliza mkataba na Geita Gold ambayo inashiriki Ligi ya Championship na inaelezwa mazungumzo baina ya pande zote mbili yanakwenda vizuri huku muda wowote mchezaji huyo atatambulishwa ndani ya Coastal Union.
Kagawa ambaye ameshawahi kupita Kagera Sugar, ameliambia Mwanaspoti kuwa sio Coastal Union pekee, bali yuko kwenye mazungumzo na timu nyingine nyingi, huku kitu pekee kilichopo anaangalia kwenye ofa nzuri ili akubali kusaini.
Alisema timu zote zilizomtumia ofa zinajaribu kumshawishi ikiwemo Geita Gold.
“Nimemaliza mkataba wangu na Geita Gold, hivyo naruhusiwa kuzungumza na timu nyingine yoyote kwa mujibu wa kanuni. Kwa sasa naendelea kufanya mazungumzo na baadhi ya timu za ligi kuu na Championship, muda ukifika kila kitu kitawekwa wazi,” alisema Kagawa na kuongeza:
“Sio sawa kuweka wazi kila jambo nikiwa bado nafanya mazungumzo na timu, lakini hiyo Coastal Union ni miongoni mwa timu ambazo zimenipa ofa.”