Wahenga wanatuasa kuwa elimu ni ufunguo na pia, katika kuisaka, hakuna mwisho. Elimu, kama hewa, iko mahali popote.
Inaweza kutoka au kutolewa na au kwa yeyote ilmradi mhusika awe tayari kujifunza na kufundisha. Hivyo, wanandoa, nao, kama waja, wana jukumu la kujifunza.
Katika maisha, kuna vitu vidogo lakini vyenye thamani ambavyo hatuvijui tupaswavyo kufundishwa au kufundisha. Vitu hivi vidogo vinaweza kusababisha makubwa yawe mabaya au mazuri. Mwanandoa awe tayari kujifunza na kufundisha.
Hivyo, kabla ya kuwa mwalimu lazima uanze kuwa mwanafunzi. Na mwalimu wako si lazima awe na shahada au kusomea ualimu. Yeyote anaweza kukufundisha, na baadaye nawe ukamfundisha. Haya ndiyo maisha. Ni nipe nikupe.
Katika kujifunza na kufundisha, tofauti na shuleni, wanandoa hawapati wala kutiana adabu wala kutoa adhabu. Hawapeani alama za ushindi au kushindwa. Kinachozingatiwa ni faida za kujifunza na kufundisha ili kuwapo amani, ufanisi, na upendo vya kweli baina ya wawili.
Kujifunza hata kufundisha haviepukiki kwa wanandoa hasa ikizingatiwa kuwa, wanapopata watoto, hugeuka uwili yaani waalimu na wazazi. Je kama hawako tayari kufundishana na kujifunza, wanawezaje kuwafundisha watoto wao?
Pia, katika kujifunza na kufundisha, kunahitajika uvumilivu wa hali ya juu hasa ikizingatiwa kuwa wanadoa siyo watoto wadogo wanaoweza kutishwa au kuogopa kuadhibiwa.
Mfano mwingine kutoka kwenye ndoa yetu ni tabia Nkwazi ya kudhani kila mtu alikuwa akijua na kuelewa kama yeye. Kabla ya kuoa, Nkwazi alikuwa na uthubutu hata wa kumwambia mtu aliyekuja kumtembelea aondoke kwa vile alikuwa amechoka na kutaka kupumzika.
Tabia hii ilimchukiza Nesaa. Aliamua kuikabili na kusema wazi kuwa ilikuwa mbaya. Taratibu, tuliua tabia hii yenye kuwaumiza wengine hata kama ilikuwa inaweka huru.
Tuligundua kuwa maisha ni kubebeana mizigo na kutoa na kupokea baadhi ya haki. Hivyo, ghafla, yalitokea mabadiliko kutokana na msukumo wa Nesaa.
Kuna mifano mingi. Binadamu, siku zote, ni mwanafunzi, ndiyo maana wahenga walisema elimu haina mwisho na haipatikani darasani tu. Maana, dunia ni darasa tosha na maisha ni mwalimu tosha.
Kama tuko radhi kujifunza toka kwa wanyama, majira, ndugu na marafiki, tunashindwa nini kujifunza kutoka kwa wenza wetu?
Wengine wanaweza kukudanganya au kukupoteza au kutokupa uzito. Lakini mwenza wako si rahisi kukupoteza au kukupuuzia kama kweli anajua thamani ya ndoa.
Maana, kila upatacho ni chenu wote. Ni kwa faida yenu. Na isitoshe, ukiharibikiwa, naye anaharibikiwa, kadhalika ukifanikiwa, wote mnafanikiwa.
Je, katika maisha ya kisasa ya tamaa na haraka, nani anakaa kumchunguza mwenziwe na kumweleza anavyomwona katika tabia na hulka? Pigilia mstari hapo, hujachelewa. Msome mwenzio na mueleze unavyomchukulia.
Hii ilitukumbusha wanandoa fulani ambapo mmoja alipata ugonjwa wa meno na jino moja kuoza. Mwenye kuoza jino lililokuwa likitoa harufu, alipenda sana kubusiwa. Mwenziwe alivumilia yote, na hatimaye akamshauri wakang’oe jino na kero ikaishia hapo hapo!
Je, ni wangapi wanajikuta katika hali hizi wanaishia kupeana migongo badala ya kulikabili na kulieleza tatizo na kulitatua? Jambo la kushangaza ni kwamba aliyekuwa anaugua jino hakuwa akijua adha aliyokuwa akiipata mwenziwe zaidi ya kulalamika maumivu tu!
Ukiona mwenzio ana tatizo au udhaifu mkabili na msaidiane kutafuta jibu. Naye mwenzio anapoelezwa asichukulie kama anavunjiwa heshima. Ni nani anaweza kujichukia kwa sababu amegundua ana kidonda mwilini mwake?
Sisi tulijijengea utaratibu wa kuandikiana barua za kesi wakati wa kutoelewana. Anayehisi amekosa au amekosewa humwandikia barua mwenziwe na kuiweka ama kitandani au sehemu tuliyokubaliana na kutoka ili mwenzake apate kuisoma na hatimaye ama kujibu au kuanzisha mjadala juu ya tatizo na chanzo cha kutoelewana.
Kumbuka tunaofanya hivyo hatuishi vyumba tofauti. Tunaisha chumba kimoja na kulala kitanda kimoja lakini bado tunaandikiana barua. Njia hii imeonyesha maajabu.
Maana, kila mtu anapokuwa anaandika huwa yuko huru na pekee. Hivyo uwezo wake wa kufikiria unakuwa mkubwa ukilinganishwa na wa yule anayejitetea mbele ya mtu mwenye hasira anayeongeza maneno au hasira. Ijaribu uone.