KOCHA wa Burkina Faso, Issa Balbone amesema viwango vilivyoonyeshwa na nyota wa Taifa Stars, Feisal Salum ‘Fei Toto’ na Yusuf Kagoma, ndiyo sababu ya kuanza vibaya katika michuano ya Fainali za Ubingwa wa Mataifa Afrika kwa wachezaji wa Ligi za Ndani (CHAN).
Timu hiyo ilianza vibaya michuano hiyo baada ya kuchapwa mabao 2-0, katika mechi ya ufunguzi kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, yaliyofungwa na Abdul Suleiman ‘Sopu’ kwa penalti dakika ya 45 na Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ dakika ya 71.
Akizungumza na Mwanaspoti baada ya mechi hiyo, Issa alisema ubora wa viungo wa Stars wakiongozwa na Kagoma na Fei Toto uliwanyima nafasi ya kutengeneza mashambulizi, japo wamejifunza kutokana na makosa na wanaenda kujirekebisha tena upya.
“Ni wachezaji wazuri sana ambao waliziba mianya ya sisi kutengeneza mashambulizi zaidi, kwa kifupi eneo lote la katikati ya uwanja walitawala, huu ni mwanzo na isitoshe michuano ndio imeanza, hivyo bado safari ni ndefu mbele,” alisema Issa.