BAADA ya Burkina Faso kuchapwa mabao 2-0 na Tanzania katika mechi ya ufunguzi ya CHAN, kocha wa timu hiyo, Issa Balbone amesema sababu kubwa ni kuchelewa kufika Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya mechi hiyo, Balbone amesema timu hiyo ilichelewa kufika Dar es Salaam hali iliyosababisha wachezaji kushindwa kucheza vizuri.
“Tulifika hapa siku mbili kabla ya mechi husika, jambo ambalo kwa kiasi kikubwa limetuathiri kwa sababu ya kushindwa kupata muda mrefu wa kuendana na mazingira husika,” amesema.
Licha ya kauli hiyo, lakini Balbone amesifu ubora wa nyota wa Stars, huku eneo la kiungo likionekana kumvutia zaidi katika mechi hiyo ya ufunguzi kundi B.
“Walicheza vizuri eneo la katikati na kutunyima nafasi ya kutengeneza mashambulizi kama tulivyotarajia, siwezi kusema kucheza kwao nyumbani imewasaidia, ila nawaponga kwa hilo,” amesema.