Unguja. Wakati kesho, Agosti 4, 2025, watiania wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wakitarajiwa kupigiwa kura za maoni, majimbo haya yatakuwa na kivumbi na jasho kwenye nafasi za uwakilishi visiwani Zanzibar.
Kura za maoni hizo zitahitimisha siku nne za hekaheka na mshikemshike wa watiania hao kufanya kampeni za kujitambulisha na kuomba kura kwa wajumbe katika maeneo mbalimbali.
Ushindani unaotarajiwa kujitokeza kwa majimbo katika nyanja tofauti, zaidi hasa maeneo ambayo kuna vigogo, wakiwemo wawakilishi wanaomaliza muda wao, lakini kuna sura mpya zenye majina maarufu zinazokwenda kuchuana kwenye mchakato huo.
Katikati ya ushindani huo, majimbo ya Kiwani na Donge wagombea wake hawatakuwa na kibarua kigumu, kutokana na Kamati Kuu kuwarejesha majina yao pekee. Hivyo, watapigiwa kura za ndiyo au hapana.
Jimbo la Kiwani mtiania pekee ni Hemed Suleiman Abdulla, ambaye ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar. Wakati jimbo la Donge, jina lililorudi ni la mwakilishi anayemaliza muda wake, Dk Khalid Salum Mohamed, ambaye ni Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi.
Miongoni mwa majimbo yanayotarajiwa kuwa na ushindani mkubwa kwenye mchakato huo ni Kikwajuni, ambapo mwakilishi anayemaliza muda wake, Nassor Salim Ali (Jazila), atachuana na Abdalla Ibrahim Natepe, aliyekuwa Katibu Tawala Wilaya ya Biharamulo mkoani Kagera.
Licha ya jimbo hilo kuwa na majina matano ya makada waliorejeshwa, lakini ushindani mkubwa unatajwa kwa wawili hao.
Ukiachana na Kikwajuni, shughuli nyingine pevu itakuwa katika jimbo la Malindi, litakalowakutanisha mwakilishi anayemaliza muda wake, Mohammed Ahmada Salum, atakayekabiliana na ushindani mkubwa kutoka kwa Mahmoud Mohamed Mussa, ambaye ni Meya wa Jiji la Zanzibar.
Siyo Malindi pekee, bali jimbo la Mpendae nalo hakupoi, ambapo mwakilishi anayetetea nafasi hiyo, Shaaban Ali Othman, ambaye pia ni Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi, atachuana na Shaib Khamis Shaib, ambaye ni Mhasibu Ofisi ya Rais Ikulu. Wawili hao watachuana na wenzao watano.
Katika jimbo la Jang’ombe, mwakilishi anayemaliza muda wake, Ali Abdugulam Hussein, ambaye pia ni Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, inaelezwa atakutana na upinzani mkali kutoka kwa Yussuf Khamis Yussuf, ambaye ni mwandishi wa habari mkongwe.
Katika jimbo la Kwahani, mwakilishi anayemaliza muda wake, Yahya Rashid Abdulla (Mamba), atachuana na Beshuu Abdalla Shaaban, ambaye ni mtaalamu wa masuala ya uchumi.
Mchambuzi wa siasa za Zanzibar, Rashid Khamis Khamis, amesema: “Ngome zilizokuwa zikitegemewa, majina hayakurudi, kwa hiyo yapo baadhi ya majimbo ushindani utapungua.”
“Ingawa katika majimbo hayo, lazima ushindani uwe mkubwa zaidi, kulingana na asili ya wagombea,” amesema.
Kwa upande wake, Ali Makame amesema kwenye uchaguzi, majimbo yote yanakuwa na ushindani isipokuwa majimbo ambayo yamerejea jina moja, ambapo mtiania anapigiwa kura za ndiyo au hapana.
Amesema majimbo mengine yatakayokuwa na ushindani zaidi ni yale ambayo majina ya wawakilishi waliokuwapo hayakurudi. Lakini majimbo ambayo hayatakuwa na ushindani ni yale wawakilishi wake walijitahidi kufanya maendeleo makubwa.
“Kisiasa, kama kuna watiania zaidi ya mmoja, basi majimbo yote yana ushindani isipokuwa alipopita bila kupingwa,” amesema Makame.
Kwa mujibu wa Makame, majimbo ya Unguja yana ushindani zaidi kuliko ya Pemba, akidai kuwa watiania wengi wamejipanga zaidi kisiwani Unguja.
Mchambuzi huyo amefafanua kuwa, majimbo ambayo wawakilishi waliomaliza muda wao na majina yao yamerudi, lakini wanadaiwa kutofanya vizuri katika utawala wao, huenda wakakumbana na changamoto.
Makame amedai kuna uwezekano baadhi ya wawakilishi wanaomaliza muda wao, majina yao yamerejeshwa na watapigiwa kura za maoni, lakini wakakosa kutokana na ushindani ulivyo.
“Si ajabu wawakilishi wa zamani asilimia zaidi ya 10 wasirudi, au ukakuta nusu kwa nusu – wapya na wa zamani. Kwa sababu kuna shida moja, watu wakiingia Baraza la Wawakilishi wanajisahau, wakiamini fedha zao zitawarejesha,” amesema.
Hata hivyo, Makame amesema mfumo wa chama uliotumika na mazingira ya kudhibiti rushwa vimesaidia kutopenyeza vitendo hivyo kwa wajumbe, licha ya kwamba haiwezekani kuzuia kwa asilimia 100.
Makame amesema Baraza la Wawakilishi lijalo linaweza likatoa mabadiliko makubwa ya demokrasia na litakuwa na uhamasishaji mkubwa kwa wawakilishi na wabunge kuwajibika kwa kuhofia kupoteza nafasi zao katika uchaguzi ujao.
Wawakilishi walioshindwa kupenya
Mawaziri walioshindwa kuchomoza katika mchakato huo ni pamoja na Waziri wa Maji, Nishati na Madini, Shaib Hassan Kaduara, ambaye ni mwakilishi wa jimbo la Chakechake Pemba.
Waziri mwingine ni Waziri wa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Idara Maalum za SMZ, Masoud Ali Mohamed, ambaye pia ni mwakilishi wa jimbo la Ole anayemaliza muda wake.
Katika orodha hiyo, wajumbe wengine wa Baraza la Wawakilishi ambao sura zao hazijaonekana ni mwakilishi wa Magomeni, Jamal Kassim Ali, ambaye pia aliwahi kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Fedha na Mipango, kisha akawa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Ikulu, kabla ya uteuzi wake kutenguliwa.
Jimbo la Tumbatu, alikuwa mwakilishi wake Haji Omar Kheri, ambaye jina lake halikurudi, badala yake yamerejea majina mengine mawili – Mohamoud Omar Hamad na Mtumweni Ali Saleh.
Mwakilishi mwingine ambaye jina lake limeenguliwa ni jimbo la Mkoani, Abdulla Khamis Kombo, ambaye pia alikuwa Mwenyekiti wa Baraza la Wawakilishi.
Mwingine ambaye amekatwa ni mwakilishi anayemaliza muda wake jimbo la Chumbuni, Miraji Khamis Mussa.