Mgaboni kupishana na Mnigeria Tabora United

UONGOZI wa Tabora United uko katika mazungumzo ya kuachana na aliyekuwa kipa wa kikosi hicho, Mgaboni Jean-Noel Amonome, ikiwa ni muda mfupi tu tangu ifikie makubaliano ya kumsajili Japhet Opubo aliyetokea Lobi Stars FC ya Nigeria.

Amonome aliyecheza timu za FC 105 Libreville ya kwao Gabon, AmaZulu FC, Royal Eagles na Uthongathi FC za Afrika Kusini, alijiunga na Tabora United dirisha dogo la usajili msimu uliopita 2024-2025, akitokea AS Arta/Solar7 ya Djibouti na kusaini mkataba wa mwaka mmoja.

Licha ya kusaini mkataba wa mwaka mmoja, lakini kipa huyo ametumikia miezi sita tu na sasa amebakisha mingine sita, ingawa mazungumzo ya kusitisha yanaendelea.

Mwanaspoti limepenyezewa taarifa kwamba kipa huyo atasitishiwa mkataba wake, ambapo anatafutwa mwingine wa kusaidiana na Japhet aliyewahi kuzichezea, Enugu Rangers IFC, Nembe City FC, Bayelsa United, FC Heartland na Sunshine Stars za kwao Nigeria.  “Hatuna shaka na makipa wazawa lakini katika mapendekezo yaliyopo mezani ni kutafuta wa kigeni atakayeleta ushindani kwa Japhet, tunahitaji kufanya vizuri zaidi msimu ujao, ndio maana tunatafuta pia wachezaji wakubwa,” kilisema chanzo hicho.

Licha ya Tabora kumtambulisha Japhet na beki wa kulia John Lazarus kutoka Lobi Stars ya Nigeria, lakini Mwanaspoti linatambua uongozi wa kikosi hicho umekamilisha usajili wa Mudathir Nassor, Abdul Latif Shauri ‘Camavinga’ na Harouna Shaban Abdallah ‘Boban’ waliotokea Zimamoto FC ya visiwani Zanzibar.

Wengine waliojiunga na kikosi hicho ni beki, Ali Juma Maarifa ‘Mabata’ aliyetokea Uhamiaji FC na kiungo, Suleiman Juma Kidawa ‘Pogba’ aliyetoka Mlandege FC, huku nyota wa kigeni ni Mkameruni, Palai Mba Manjie aliyetoka Victoria United FC.